EPL inahitaji mtoano kushuka daraja

Tuesday May 15 2018

 

HATIMAYE Ligi Kuu England (EPL) imemalizika kwa machungu na matamu yake kulingana na jinsi timu zilivyokuwa zimejiandaa na kufanya uwanjani.

Wapo walioshuka, waliotwaa ubingwa na waliofuzu kwa mashindano mawili ya Ulaya ambayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na Ligi ya Europa).

Mbio za ubingwa ni kana kwamba zilifungwa mapema kiasi kutokana na umiliki na udhibiti wa Manchester City tangu mwanzoni mwa msimu, ikiacha pengo kubwa kwa washindani wake. Hakuna aliyewasogelea, si Manchester United, Tottenham Hotspur, Liverpoool, Chelsea wala Arsenal. Hakuna.

Pep Guardiola, kwa hiyo, amemaliza msimu wake wa pili nchini England kwa raha, akianza kufananisha mafanikio hayo na yale ya Hispania alikokuwa na Barcelona na Ujerumani alikokuwa na Bayern Munich. Kote aliwapa mafanikio.

Wakati ushindani huko juu – kwenye ubingwa ulikuwa mdogo, kule chini katika mbio za kujiepusha na kushuka daraja hapakuwa salama, kwa sababu masahibu yalikuwa mengi na kwa timu nyingi.

Ilifika mahali baada ya mzunguko wa pili kuanza, kukawa na hofu miongoni mwa timu karibu zote zilizokuwa chini ya nusu ya jedwali la msimamo wa EPL. Na sasa, baada ya kushuka hata zile timu ambazo zilikuwa tishio kwa vigogo, zikiitwa wagumu wa ligi – Stoke na West Bromwich Albion, nani tena anaweza kuwa salama?

Kushuka ni kushuka tu wala hakuna shida, lakini nani anayeshuka ndiyo tabu, kwa sababu kushuka kuna hasara zake nyingi sana kisoka, kisaikolojia, kijamii na kiuchumi. Wapo wanaoshuka kwa ‘bahati mbaya’ kutokana na uamuzi mbaya labda kwenye mechi chache kama ambavyo timu yaweza kutwaa ubingwa kibahati tu.

Nakumbuka Manchester City ya Roberto Mancini walivyotwaa ubingwa kwa bahati ya mabao ya baadaye sana, huku Sir Alex Ferguson upande mwingine akiwa anaangalia saa na kujaribu kupata matokeo ya ‘wapiga kelele’ hao wakati mechi ikielekea kuisha, kwa sababu ya tofauti ndogo mno ya pointi au alama.

Hata kwa Tanzania msimu ule mwingine Yanga walitwaa ubingwa dhidi ya Simba kwa ajabu dakika za mwishoni, wakitofautiana kidogo sana. Labda sasa utaratibu ubadilishwe huku na huko nyumbani pia.

Napenda ule wa Ligi Daraja la Kwanza au Championship hapa England, ambapo kupanda daraja kuingia EPL si mchezo. Ukishika nafasi ya kwanza ndio unajihakikishia kupanda, lakini kuanzia wa pili kwenda chini lazima muende kwenye mechi za mtoano, maarufu kama play-offs.

Nadhani huo ni utaratibu mzuri ili kupata kilicho bora zaidi kutoka kwa walio bora. Sasa utaratibu huo naona ni bora ungeingizwa kwenye EPL – kwa wanaochukua ubingwa kwa alama nyingi ni ngumu kuwapambanisha tena, kwa hiyo wanabaki kuwa wao.

Lakini katika kuwania nafasi tatu zilizobaki, iwe bora kwamba wapambanishwe timu wenye alama za kukaribiana sana kwa play-offs; zinaweza kuwa timu sita au hata saba kulingana na alama zilivyo, ili mbali na bingwa, wapatikane wawakilishi wa kweli kwenye UCL.

Lakini kwa upande mwingine, kwenye kushuka, ili haki itendeke lakini pia ionekane inatendeka ni muhimu kuwa nao. Timu za kule (mkiani) hufika mahali zikatofautiana kwa alama kidogo mno na kushuka daraja kuna majanga yake.

Tazama sasa kabla ya mechi ya mwisho wikiendi iliyomalizika timu za mkiani hazikuwa zinapishana sana; Stoke waliingia mechi ya mwisho wakiwa na alama 30 wakati West Brom wakiwa na 31, Swansea 33, Southampton 36 na Huddersfield 37.

Hapo juu yao tu walikuwa ni West Ham na alama 39, Brighton 40 na hata ukipanda hadi nafasi ya 10 – nusu ya jedwali kulikuwapo Newcastle wenye alama 41. Tofauti kidogo sana ya alama hizi kwa hiyo si sawa kusema huyu hafai na yule anafaa. Wafike mahali wakuu wa soka waamue kwamba kabla ya watatu kushuka, basi waliozoeana kwa namba wachezeshwe mechi za mtoano nyumbani na ugenini ili kupata washindwa kweli na washuke daraja.

Badala ya kufikiria tu masuala kama kuuza Uwanja wa Taifa – Wembley, wakuu wanatakiwa sasa kujielekeza kwenye mambo mazito kama haya na pia iwe hivyo kwa Afrika Mashariki ili bingwa kweli atokwe jasho na wanaoshuka daraja hakika wawe wametumia kila walicho nacho na kushindwa kuhimili kubali juu.