Were ategwa Harambee Stars

KOCHA wa timu ya soka ya taifa, Harambee Stars, Adel Amrouche

Muktasari:

  • Were ana rekodi nzuri anapovaa jezi ya Tusker na kwa sasa ndiye anayeongoza kwa upachikaji mabao kwenye Ligi Kuu Kenya akiwa ametikisa nyavu mara 14.

KOCHA wa timu ya soka ya taifa, Harambee Stars, Adel Amrouche, amemtega mshambuliaji Jesse Were akimtaka aongeze bidii zaidi anapoichezea Stars ili afanane na namna afanyavyo anapoicheza klabu yake, Tusker FC.

Amrouche alisema hauo alipotaja kikosi chake cha wachezaji 27 akiwamo Were kwa ajili ya kuanza mazoezi kujiandaa kwa mechi ya kusaka tiketi ya fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Namibia. Mechi hiyo itachezwa wikiendi.

Were ana rekodi nzuri anapovaa jezi ya Tusker na kwa sasa ndiye anayeongoza kwa upachikaji mabao kwenye Ligi Kuu Kenya akiwa ametikisa nyavu mara 14.

Akizungumzia mchezaji huyo, Amrouche, alisema ijapokuwa Were anang’aa sana akiwa Tusker msimu huu, anatakiwa  kutia bidii katika timu ya taifa.

“Jesse Were anafahamu bayana mtazamo wangu wa mchezo wake. Kila mara ninamweleza kwamba anaweza kufunga mabao mengi jinsi anavyofanya katika klabu,” alisema.

“Lakini  anapokuwa na kikosi cha taifa atahitaji kupigania mpira zaidi. Ni fursa yake sasa kwani Stars inahitaji  mshambuliaji stadi.”

Wakati huohuo, Amrouche amesema atatafuta ushindi dhidi ya Namibia licha ya kwamba mechi hiyo haina faida kimatokeo kwani kikosi chake kimeshapoteza nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya Kundi F.