Yanga, mbona kazi wanayo!

Muktasari:

  • Mwanaspoti linachukua juhudi za kuwatafuta baadhi ya wajumbe kutaka kujua mikakati na namna watakavyoubeba msalaba huo wa kuiona Yanga inapaa zaidi.

SOKA la sasa nguvu yake kubwa ni fedha na mipango ya kisayansi zaidi, asikuambie mtu. Achana na blahblah za kuwa soka ni burudani tu na ujanja ujanja tu. Kama timu haina fedha wala mipango mizuri ni ngumu kuhimili vishindo katika michuano yoyote. Waulize Majimaji ya Songea watakuambia, watafute Africans Sports ama Villa Squad zilizowahi kucheza Ligi Kuu watakujibu. Hata Toto Aficans ya Mwanza wanalijua hili vyema kabisa.

Kwa kutambua kuwa ili timu iweze kuvuna mafanikio katika michuano yoyote ni lazima iwe na safu nzuri ya kiufundi.  Bosi wa Yanga Yusuf Manji, hivi karibuni alifanya uteuzi wa Kamati ya Mashindano, ikiwa ya kwanza kuiunda tangu arejee tena madarakani. Kamati hiyo itakuwa na jukumu la  kusimamia mashindano mbalimbali.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mhandisi Paul Malume aliyechukua nafasi ya Isaac Chanji aliyemaliza muda wake, ikiwa pia imejumuisha vigogo 18 ambao, wanabeba dhamana ya kuendeleza timu hiyo ilipoishia msimu uliopita.

Mwanaspoti linachukua juhudi za kuwatafuta baadhi ya wajumbe kutaka kujua mikakati na namna watakavyoubeba msalaba huo wa kuiona Yanga inapaa zaidi.

Paul Malume (Mwenyekiti)

Malume ambaye anaingia katika kamati hiyo kwa mara ya kwanza anazungumzia uteuzi huo akisema: “Uteuzi huo kwangu kuongoza kamati hii nimeupokea kwa nguvu moja kwa kuwa ni mdau mkubwa wa Yanga.

“Majukumu yetu kama kamati tunayajua la kwanza ningependa ushirikiano ndani ya klabu ukitangulizwa mbele kwa kuwa hii ni timu yetu sote, ningependa zaidi tuwe na timu bora itakayomudu ushindani wowote ndani na nje ya nchi.

“Tuseme ukweli Yanga ina uwezo mkubwa, tuna fedha, wachezaji wazuri na hata makocha wazuri sasa sioni sababu ya kutofanya vizuri nafikiri tutakuwa timu bora zaidi.”

Lengo Kuu ni lipi?

“Lengo kuu hapa Yanga sasa ni moja tu, kwa kuwa tumeshapata uzoefu wa kutosha katika mashindano ya kimataifa kama ambavyo tulishiriki msimu uliopita, niwapongeze wenzangu waliofanya kazi hii kabla yetu hasa Chanji na kamati yake wakisaidiana na uongozi wa juu.

“Tunachotakiwa kufanya na kamati yangu ni kuhakikisha tunashinda Kombe la Afrika katika msimu ujao.

Samuel Lukumay (Katibu wa Kamati)

Wakati Malume akifafanua hayo kwa upande wake, Lukumay ambaye ni mzoefu katika kamati hii akitangulia katika kamati zilizopita anasema; “Kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyekiti wangu Malume kwa kunipa nafasi hii akitambua uzoefu nilionao, pia nisiwasahau Wanayanga ambao walitangulia awali kunichagua kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji.

Wanalenga kufanya nini

“Kimsingi mwaka jana nilikuwa mjumbe wa Kamati ya Mashindano na tumepambana kwa hali na mali tukishirikiana na uongozi wa juu na hata kamati yetu iliyopita chini ya Chanji tulifanikiwa kuchukua makombe yote ya ndani, pia tukafika hatua ya makundi Kombe la Shirikisho na sasa hapa tuna moja tu ikiwezekana tuchukue kombe kabisa kutokana na ubora wetu.

“Kamati hii jukumu letu sio kuendesha timu, tumepanga kuwa karibu na timu yetu na kufanyia kazi yale yote yatakayopendekezwa na benchi la ufundi kuanzia maandalizi ya timu na kuhakikisha timu inashinda mechi katika mashindano yote tutakayoshiriki.

Nini kifanyike Yanga ipae zaidi

“Kikubwa ni kuwa na timu bora yenye ushindani na sasa tuna kikosi imara, lakini pia tunachotakiwa kukifanya ni kuona masilahi ya wachezaji yakikamilishwa kwa wakati. Tumejipanga na hayo naamini chini ya utawala wa Manji na makamu wake Clement Sanga na wajumbe wenzangu tutayafanikisha.

Tukumbuke tu hivi karibuni, kocha wetu aliamua timu ifanyie mazoezi katika uwanja wa Kaunda pale Jangwani wengi walitubeza wakisema tumefilisika, lakini hiyo ni sehemu ya utaalamu ambao kocha aligundua aina ya uwanja ambao tunakwenda kuutumia hauna tofauti kubwa na ule wa Kaunda na matokeo yake tumeshinda vyema sasa mambo kama haya ndiyo tunataka kuona yanafanyika sasa tathmini za kina zinafanyika ili tuweze kushinda kokote ligi ya mwaka huu ni ngumu Wanayanga watuamini tutapambana kwa ajili yao.

Yusuphed Mhandeni (Mjumbe)

Ndani ya Yanga jina la Yusuphed Mhandeni ni linafahamika sana kwa kuwa mtu wa kujitolea mara kwa mara katika safari za timu hiyo ndani na nje ya nchi ambapo, umuhimu wake ukampa nafasi Manji kuona ni mtu sahihi wa kuwepo kwenye kamati hiyo ili kunogesha zaidi.

Manji kawapa kazi gani?

“Jukumu alilotupa Manji ni kubwa lakini linawezekana kama tukifanya kazi kwa pamoja na ushirikiano. Nakumbuka katika kikao chetu cha kwanza wakati akitukabidhi jukumu hili alituambia wazi kwamba, ametuchagua ili tuisaidie Yanga na sio kusubiri Yanga itusaidie sisi, hii ni kauli ambayo utagundua jukumu letu ni lipi katika timu na sasa tumeanza kazi ambayo tumeagizwa kuifanya.

Yanga imejifunza nini Shirikisho?

“Nafikiri kila kitu kilionekana, kwanza tulikuwa ya timu imara, lakini uzoefu mdogo ndio uliotuangusha sasa tunajipanga kuhakikisha katika Ligi ya Mabingwa mwakani hatufanyi makosa tena tunataka kuona makubwa yakifanyika.

“Unapokuwa katika mashindano ya kimataifa kuna mengi ya tofauti unakutana nayo, fitna ni nyingi ambazo hapo awali tulikuwa hatujazipitia hapa ndani kuna changamoto zake ambazo ni tofauti kabisa na zile za nje, sasa tumejua kila kitu dhamira yetu sasa ni kuona makubwa yakifanyika katika kipindi cha uongozi wetu tukishirikina na wenzetu wa juu.