Ngoma Simba, Ajib Yanga

Muktasari:

Hali ngumu ya maisha katika utawala wa Rais John Magufuli umepelekea timu za Simba na Yanga kushindwa kuwapiga pingu mastaa wake wakubwa jambo ambalo linawaacha huru kuchagua timu ya kujiunga nazo punde msimu utakapomalizika.

SIMBA au klabu nyingine yoyote kikanuni inaweza kufanya mazungumzo na Donald Ngoma wa Yanga na kuandikishana naye wakati wakisubiri msimu umalizike, hata Yanga inaweza kufanya hivyo pia kwa Ibrahim Ajib na Juuko Murshid.

Hali ngumu ya maisha katika utawala wa Rais John Magufuli umepelekea timu za Simba na Yanga kushindwa kuwapiga pingu mastaa wake wakubwa jambo ambalo linawaacha huru kuchagua timu ya kujiunga nazo punde msimu utakapomalizika.

Mbali na kuondoka bure mwishoni mwa msimu, mastaa hao wanaweza kuanza mazungumzo na timu yoyote sasa na kufikia makubaliano ya awali ili mwisho wa msimu waweze kumwaga wino na kuanza maisha mapya kama zinavyofanya klabu nyingi zilizoendelea.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya mastaa wa Simba na Yanga ambao, kandarasi zao zinamalizika mwishoni mwa msimu na wanaweza kupatikana bure.

 

Jonas Mkude, Simba

Nahodha wa Simba, Jonas Mkude atapatikana bure tu mwishoni mwa msimu. Kama una mkwanja wako wa maana unaweza kuanza mazungumzo na kiungo huyo wa Simba na punde akimaliza msimu ataweza kuungana na timu yako kwa ajili ya maisha mapya.

Mkude aligoma kuongeza mkataba mpya Simba kwa madai kuwa maslahi wanayompa ni kidogo hivyo, kuomba kuondoka kama mchezaji huru mwishoni mwa msimu kwa madai kuwa amepata timu nje ya nchi.

Taarifa kutoka Simba zinadai kuwa wameingia makubaliano maalum na staa huyo na ikitokea akakosa dili la nje hataweza kujiunga na timu nyingine ya hapa nchini tofauti na Simba.

 

Donald Ngoma, Yanga

Usiumize kichwa. Staa wa Yanga, Donald Ngoma anapatikana. Ngoma aliyesajiliwa na Yanga kwa dau la zaidi ya Sh 90 milioni amegomea mkataba mpya klabuni hapo jambo ambalo litamfanya awe mchezaji huru mwishoni mwa msimu.

Kwa kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), timu yoyote inaweza kuanza mazungumzo na staa huyo kuanzia mwezi ujao ambapo, atakuwa amesaliwa na miezi sita tu katika mkataba wake wa sasa.

Habari za ndani zinadai straika huyo hafurahishwi na maisha yanavyokwenda ndani ya Yanga hasa kucheleweshwa mishahara mara kwa mara tangu miezi ya mwishoni mwa mwaka jana pamoja kutokuwepo kwa mawasiliano ya kuridhisha kati yake na viongozi wa juu. Kwa sasa yupo kwao kwa maelezo kwamba amepatwa na msiba wa ndugu yake, ingawa baadhi ya watu wa Yanga wanadai amekwenda kupumzika.

 

Juuko Murshid, Simba

Beki katili uwanjani na anayeijua kazi yake, Juuko Murshid naye unaweza kumpata. Habari zinadai kwamba Kocha wa Uganda, Sredejovic Milutin ‘Micho’ yupo kwenye harakati za kumuuza lakini bado dili haijakaa sawa. Juuko aliyejiunga na Simba mwishoni mwa mwaka 2014 amekuwa katika kiwango bora kitendo ambacho kimempa nafasi ya kuungana na kikosi cha timu ya taifa ya Uganda kilichokwenda kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Gabon. Beki huyo anayesifika kwa soka la kazi anaweza kujiunga na timu yoyote msimu ujao tena bure tu kwani, Simba mpaka sasa wameshindwa kuweka ofa ya maana mezani kwake huku akionekana akili yake imeanza kuangalia maisha mapya nje ya Msimbazi.

 

Vicent Bossou, Yanga

Baada ya kushindwa kuachana na Yanga katika dirisha dogo la usajili lililofungwa mwezi ulipita, Vincent Bossou sasa anapatikana bure kabisa. Katika usajili wa dirisha hilo dogo, Bossou alitaka kununua mkataba wake wa miezi sita uliokuwa umesalia ili aweze kujiunga na timu moja nchini Vietnam, lakini Yanga walimuwekea ngumu na kumwambia timu hiyo sio duka. Hata hivyo, habari za ndani ya Yanga zinadai kuwa anaweza kuondoka klabuni hapo muda wowote kwani, ameshamalizana na klabu moja ya Vietnam lakini hajataka kuweka mambo wazi mpaka mashindano ya Afcon yamalizike.

 

Ibrahim Ajib, Simba

Straika mwenye vitu vingi ndani ya kikosi cha Simba, Ibrahim Ajibu naye kikanuni yuko sokoni, Yanga, Azam hata Majimaji yoyote mwenye fungu la maana anaweza kumalizana naye akitaka. Ajibu, ambaye ni chimbuko timu ya vijana ya Simba amekuwa na kiwango cha wastani akiifungia timu hiyo mabao 12 katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

Chipukizi huyo amekuwa akilaumiwa kwa kucheza soka la kawaida bila kujituma jambo ambalo limeifanya Simba iwe nzito kumpatia mkataba mnono kwa madai kwamba, ameshindwa kufikia ubora ambao wanauotarajia.

Hata hivyo, bado Ajib anasalia kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wapo sokoni bure na ana kipaji cha aina yake. Si mchezaji ambaye Kocha mwenye malengo ya muda mrefu anaweza kumuachia kirahisi.

 

Mwinyi Haji, Yanga

Beki wa kushoto mwenye roho ya paka ni chaguo la kwanza katika kikosi cha Yanga na Taifa Stars yupo katika miezi sita ya mwisho katika mkataba wake na timu inayomhitaji inaweza kumpata.

Mwinyi amekuwa katika kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu ambapo, makocha Hans Van Pluijm na George Lwandamina wamekuwa wakimpa kipaumbele katika kikosi cha kwanza.

 

Janvier Bokungu, Simba

Aliingia Simba kama mchezaji wa kawaida sana na hata usajili wake ulifanyika kawaida pia, viongozi wakijaza nafasi ili kuangalia uwezekano wa kufanya mabadiliko ndani ya dirisha dogo la Desemba.

Lakini hapo katikati akabadilika na kuwadhihirishia kwamba, mawazo waliyokuwa nayo sio sahihi. Anapatikana bure mwisho wa msimu. Beki huyo ambaye alipiga penalti ya kistaa katika mchezo dhidi ya Yanga kwenye kombe la Mapinduzi, anapatikana bure baada ya msimu kufikia tamati.

 

Haruna Niyonzima, Yanga

Niyonzima ambaye ni mchezaji ghali zaidi katika kikosi cha Yanga yupo katika miezi sita ya mwisho ya mkataba wake na kama unahitaji huduma yake unaweza kuzungumza naye na kufikia makubaliano maalum kisha akahamia katika timu yako mwishoni mwa msimu.

 

Wengineo

Mastaa wengine ambao mwishoni mwa msimu watakuwa wachezaji huru ni mastraika wa Yanga, Matteo Anthony, Malimi Busungu pamoja na kiungo Thabani Kamusoko huku kwa upande wa Simba kiungo mkongwe, Mwinyi Kazimoto mkataba wake pia uko ukingoni kabisa hivyo, kazi kwenu.