Lwandamina anavyoteseka

Monday March 20 2017

 

By GIFT MACHA

WAKATI mwingine maisha huwa yanaambatana na changamoto nyingi tu. Kuna changamoto ambazo huwa ndani ya uwezo wa mhusika lakini nyingine huwa huwa nje ya uwezo wake. Hapo ndio huwa balaa.

Ni wazi kocha wa Yanga, George Lwandamina, ana maisha magumu ndani ya Yanga, japo si sana. Katika kipindi cha miezi mitatu aliyokaa klabuni hapo, mambo yamekuwa yakigoma kabisa kwenda katika njia aliyoitazamia.

Kwanza, wakati ameanza kazi tu, kocha huyo alipoteza pointi katika mchezo muhimu dhidi ya African Lyon mwishoni mwa mwaka jana baada ya sare ya bao 1-1.

Matokeo hayo yaliifanya Yanga kuongeza tofauti ya pointi baina yao na Simba kutoka mbili hadi nne. Bahati nzuri ni kwamba kwa sasa tofauti hiyo imerudi tena kuwa mbili.

Pili, kocha huyo alikumbana na kadhia ya kipigo cha aibu cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC katika michuano ya Kombe la Mapinduzi. Ni kipigo kikubwa zaidi kwa Yanga tangu ilipofungwa mabao 5-0 na Simba Mei, 2012.

Baada ya hapo Lwandamina alijikuta akipoteza mechi mbili dhidi ya Simba ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na nusu tu. Alipoteza mchezo wa kwanza kwa mikwaju ya penalti visiwani Zanzibar kabla ya kipigo cha mabao 2-1 hivi karibuni.

Mbaya zaidi ni kwamba baada ya Simba kupoteza pointi katika sare ya mabao 2-2 na Mbeya City, Yanga ilishindwa kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kutoka suluhu na Mtibwa Sugar. Bahati mbaya iliyoje.

Hali mbaya zaidi kwa Lwandamina ni baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika na kutupwa Kombe la Shirikisho.

Yanga ilitolewa na Zanaco baada ya sare ya 1-1 Dar es Salaam na Lusaka, Zambia ikatoka suluhu na kuipa Zanaco faida ya bao la ugenini.

Yanga sasa inasubiri kapu, ipangiwe timu icheze, ndipo iingie hatua ya makundi Kombe la Shirikisho kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Kutokana na mfululizo wa matukio yanayoendelea sasa, Mwanaspoti inakuletea tathmini ya matatizo yanayomwandama kocha huyo raia wa Zambia. Maisha ni kama yanamwonea wivu vile.

Sekeseke la Manji

Wakati Lwandamina anakabidhiwa timu tu, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, aliingia matatizoni na kushindwa kutoa sapoti ya kutosha kwa timu. Kwanza, Manji alikumbana na rungu la Mfuko wa Mafao wa PSPF ambao ulitoa nje vitu vyake vyote katika jengo la Quality Plaza. PSPF walifanya hivyo kutokana na madai yao ya pango kwa Manji kufikia Sh12 bilioni.

Wakati mambo yanataka kukaa sawa, Manji aliingia katika matatizo mengine tena hivyo kukwamisha kabisa ndoto za Lwandamina. Manji alitajwa katika kesi ya matumizi ya dawa za kulevya na  baada ya kuwekwa kizuizini kwa wiki moja alipandishwa mahakamani na kuachiwa kwa dhamana, kesi inaendelea.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Manji alihusishwa tena na umiliki wa hati mbili za kusafiria na kujikuta akirejea tena matatani.

Kutokana na Manji kuwa na matatizo, Yanga imeshindwa kuwa na maisha mazuri iliyozoea. Maisha ya kufundisha yamekuwa magumu kwa Lwandamina ambapo sasa analazimika kuweka mambo sawa kwa kutumia ushawishi binafsi.

Migomo ya wachezaji

Mwishoni mwa mwaka jana, wachezaji wa Yanga waligomea mazoezi kwa siku mbili kushinikiza malipo ya mishahara yao. Ni changamoto kwa kocha yeyote. Lwandamina alifika mazoezini na kujikuta akiwa na wasaidizi wake tu, wachezaji hawakutokea.

Viongozi wa Yanga walifanya jitihada na kufanikiwa kumaliza mgomo huo. Hata hivyo mwaka huu kumekuwa na mfululizo wa migomo ya wachezaji pia. Vincent Bossou aligoma kucheza mechi dhidi ya Simba akishinikiza kulipwa mishahara yake ya miezi minne matokeo yake timu ikafungwa mabao mawili mepesi.

Wachezaji wengine wanadaiwa kukosa morali ya kupambana kutokana na matatizo ya mishahara kuendelea kuwa makubwa siku hadi siku. Inadaiwa kuwa wapo baadhi ya wachezaji ambao wanadai mishahara ya miezi mitatu. Timu haiwezi kufanya vizuri katika mazingira hayo.

Majeruhi kibao

Wachezaji muhimu wa Yanga wanakumbwa na majeruhi karibu kila siku. Kwa siku za karibuni; Thaban Kamusoko, Amissi Tambwe na Donald Ngoma, walikuwa majeruhi. Said Juma ‘Makapu’ alikuwa majeruhi pia jambo ambalo limesababisha Kelvin Yondani kulazimika kucheza nafasi ya kiungo.

Wachezaji muhimu wa Yanga wamekumbwa na majeruhi na kuzikosa mechi muhimu. Mfano Yanga ililazimika kucheza na Mtibwa Sugar huku ikiwakosa Niyonzima, Kamusoko, Ngoma na Tambwe. Ilikuwa ni ngumu kwao kupata ushindi.

Yawezekana Lwandamina anatoa mazoezi makali kwa wachezaji wake. Hali ya majeruhi ndani ya timu inatishia amani ya usalama wa Yanga hasa katika michuano ya kimataifa. Ni wazi kwamba benchi la ufundi linapaswa kutazama kwa kina namna ya kutatua tatizo hilo.

Ratiba ngumu

Ni wazi kwamba, Yanga imekuwa na mechi nyingi kuliko timu nyingine yoyote kutokana na ushiriki wake katika mashindano matatu. Yanga inashiriki Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, Yanga imelazimika kucheza mechi tano mfululizo jambo ambalo linaziweka nafasi zao rehani. Yanga imecheza na Simba, Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar, Kiluvya United na Zanaco.

Katika mazingira kama haya ya mechi tano kwa siku 15 unawezaje kushinda? Unawezaje kufanya hivyo hasa pindi unapokutana na timu ngumu kama Simba, Mtibwa Sugar na Zanaco? Maisha yanamwonea wivu Lwandamina.