JICHO LA MWEWE: Kina Kichuya wanahitaji mameneja wavaa suti

Muktasari:

  • Wachezaji wa kigeni wa Simba kasoro, Method Mwanjali wanaonekana wako hoi sana. Laudit Mavugo yuko hoi. Alitisha katika mechi moja tu dhidi ya AFC Leopards siku ya kwanza Simba walipokuwa wanatuonyesha jezi zao mpya. Baada ya hapo akajiona Lionel Messi au Emmanuel Okwi.

NAITAZAMA Simba imebadilika na inanivutia kweli kweli. Sijui mbele ya safari itakuwaje, lakini sidhani kama Simba hii inafanana na ile ambayo ilitoa sare sita mfululizo. Mpira hauchezwi chumbani unachezwa hadharani.

Kasoro Ibrahim Ajib na Mohamed Tshabalala, wachezaji wengi wanaoisaidia sana Simba ni wale wapya. Hii inaonyesha kwamba walifanya usajili wao vyema kuliko walivyokuwa wanafanya katika miaka ya karibuni.

Napenda kumtazama Shiza Kichuya. Mguu wake wa kushoto ni mwepesi na anacheza kwa malengo sana uwanjani. Navutiwa kumtazama Mzamiru Hassan, fundi wangu wa mpira, Mohamed Ibrahim bado hajachanganya sana.

Wachezaji wa kigeni wa Simba kasoro, Method Mwanjali wanaonekana wako hoi sana. Laudit Mavugo yuko hoi. Alitisha katika mechi moja tu dhidi ya AFC Leopards siku ya kwanza Simba walipokuwa wanatuonyesha jezi zao mpya. Baada ya hapo akajiona Lionel Messi au Emmanuel Okwi.

Fredrick Blagnon naye yupo hoi, anakosa mabao katika muvu za kawaida kabisa na anakosa na hata penalti. Sijui, lakini tuliambiwa Simba wana Muivory Coast ambaye anatisha sana. Hatufahamu nini kinatokea au Simba waliuziwa Mbuzi kwenye gunia.

Vyovyote ilivyo, Simba hii inanikumbusha Mrisho Ngassa wakati akiwa fiti na Yanga yake. Mshahara wake ulikuwa mdogo dhidi ya mastaa wa kigeni wengi aliocheza nao pale Yanga. Kina David Mwape, Ken Asamoah, Boniface Ambani na wengineo wengi aliokuwa anawatengenezea mabao au anafunga mwenyewe.

Tatizo liko wapi? Utakuta mshahara wa Mavugo ni mkubwa mara mbili ya mshahara wa Ajib au utakuta mshahara wa Blagnon ni mara tatu ya ule wa Kichuya. Jibu ni moja tu, wachezaji wetu hawajitambui sana na hawaelewi hata umuhimu wa kuwa na mameneja wavaa suti.

Kama ningekuwa Ajib, meneja wangu au wakala wangu ningehakikisha anakuwa Mnigeria, Mzambia au Mghana. Hapo ndipo heshima inapoanzia kwani, wachezaji wetu wanalaliwa sana kwa sababu wanajiwakilisha wenyewe tu mbele ya meza ya mazungumzo huku wakiwa wamezungukwa na kundi kubwa la viongozi.

Kama mchezaji akiwakilishwa na mtu, basi unakuta mtu huyo huyo ni shabiki wa Simba au Yanga, ambaye akili yake pia inabakia katika kuinufaisha timu yake badala ya kuzama na kujikita katika kumsaidia mchezaji na kujisaidia mwenyewe katika pesa yake ya juu.

Unamkuta mchezaji mwenye kipaji na uwezo mkubwa, lakini timu zetu zikimtaka zinakwenda kwa mama yake au mjomba kuzungumza naye. Mama ambaye hafahamu lolote kuhusu soka atazungumza nini zaidi ya kumshawishi mwanae asaini mkataba?

Matokeo yake wachezaji wa kigeni wanatumia fursa hizi kutengeneza ukubwa wao katika meza za mazungumzo na kupata mikataba mikubwa. Wao wanawakilishwa na mameneja wanaovaa suti, Kiingereza kingi na ufahamu mwingi wa masuala ya mikataba na kanuni za Fifa.

Hivi ndivyo viongozi wa Yanga walivyouziwa mshambuliaji wa Cameroon, Jama Mba ambaye alitinga uwanja wa ndege na meneja wake wote wakiwa na suti nene. Akapata mkataba mnene.

Mwenyekiti wa Yanga wa wakati huo, Iman Madega niliwahi kukutana naye akatamba kwamba, Mba peke yake alikuwa na uwezo wa kuwabeba mgongoni walinzi wawili wa Simba wa wakati huo, Kevin Yondani na Juma Nyosso kisha akaenda kufunga bila ya bughudha.

Siku ya kwanza kuingia uwanjani ungegundua tu kuwa Mba alikuwa kichekesho. Hata jinsi ya kumiliki mpira ilikuwa shida achilia mbali kufunga au kukokota mpira. Yote haya yalikuwa yanaendelea huku Ngassa akibakia kuwa staa wa timu na mshahara wake mdogo.

Sioni mwisho wa Simba hii kubebwa na wageni. Hapana, itaendelea kubebwa zaidi na wazawa. Tatizo ni kwamba wazawa wenyewe hawajitambui sana na kama wakijitambua watainufaisha zaidi klabu na wao wenyewe watajinufaisha zaidi.

Mchezaji kama Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ hastahili kununuliwa gari na kiongozi bali anastahili kuwa na mshahara mkubwa au posho kubwa ambazo zitamfanya anunue gari analotaka kwa pesa anayotaka bila ya kikwazo chochote kile. Tufike huko.

Kando ya Haji Mwinyi, anaweza kuwa ni mlinzi bora wa kushoto ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Je, mwenyewe anatambua hilo? Mtu anayemsaidia katika masuala ya mikataba anatambua hilo? Unaweza kukuta anajisimamia mwenyewe akiwa amevaa jeans yake tu bila kutambua kuwa anahitaji meneja mwenye suti na Kiingereza kingi ili apate mkataba mnono.

Wachezaji wetu waanze kujipima na kujielewa na hata viongozi wetu waanze kuwapima wachezaji wetu na kuwaelewa. Wakati mwingine unaweza kuchukua mshahara wa Mavugo ukauweka kwa Kichuya. Kuanzia hapo Yanga na Azam watamsikia Kichuya redioni tu na hawatampata kamwe.

Hata mchezaji anayetajwa kuwa mvivu kama Ajib dawa yake ni kumpa mitego ya pesa ambazo hawezi kuzipata kama akiendelea kuwa mvivu. Tatizo letu tunathamini sana mameneja wanaovaa suti na ndiyo maana wanatupiga pesa kupitia kwa wachezaji wa kawaida kabisa ambao, hata Tanzania wanapatikana wengi kwelikweli.