Allan Shomari: Beki kitasa aliyepata upofu kama utani

Tuesday May 16 2017

 

By YOHANA CHALLE, ARUSHA

WAKATI mwingine maisha huwa na mitihani mingi ambayo kama si Mcha Mungu na anayeamini katika dini, ni rahisi kuingia kwenye kufuru.

Mtu anaweza kuamini labda ana bahati mbaya ama anayeonewa, lakini ukweli ni kwamba kila linalompata mwanadamu hapa duniani ni mipango ya Mungu Muumba wa Mbingu na Ardhi.

Yeye ndiye mpangaji wa kila jambo kwani kwake huwa ni kitendo cha kusema ‘kuwa’ na hapohapo jambo likawa.

Nyota wa zamani wa kimataifa wa soka aliyewahi kutamba na Yanga, Allan Shomari kwa sasa haoni baada ya kupata upofu ukubwani, ni jambo linalompa changamoto kubwa.

Beki huyo kitasa wa zamani anasema kuwa hakuzoea hali hiyo, lakini hana budi kumshukuru Mungu kwani hujafa hujaumbika.

Mwanaspoti lilimtembelea nyumbani kwake jijini hapa kumjulia hali na kufanya mahojiano maalumu yaliyozaa makala haya, na amefunguka mambo mengi juu ya safari yake kisoka, mkasa wake wa kupofuka macho na mikasa mingine. Endelea naye...!

TATIZO UDEREVA

Beki huyo wa zamani aliyewahi kutamba na klabu mbalimbali nchini ikiwamo Yanga, anasema tatizo lake lilianzia kwenye shughuli yake ya udereva kazi aliyoifanya baada ya kustaafu soka.

Shomari anasema yeye ni bonge la suka (dereva), taaluma aliyoisomea mara baada ya kumaliza elimu yake ya msingi, na wazazi wake walimpeleka kujifunza udereva na kuhitimu.

Anasema hakuifanya kazi hiyo kwa sababu ya kunogewa na soka, lakini aliirejea baada ya kuachana na soka na ndipo chanzo cha tatizo lake la kupofuka macho lilipoanzia na kumpa wakati mgumu katika maisha yake, japo sasa amezoea.

Mkali huyo anasema kuwa, mara baada ya kuachana na soka aliirejea kazi yake ya magari, lakini akianza kama utingo, ili kuzoea kwanza barabara kwani ni kipindi kirefu alikuwa nje ya fani kwa sababu ya soka.

“Nilianza kama utingo kwa muda fulani, ili nizoee barabara kwani kampuni yetu ya Born City ilikuwa ikisafirisha abiria kutoka Dar, Shinyanga na baada ya kuzoea nilihamia kwenye udereva na kuifanya katika kampuni hiyo kabla ya kuhama.

“Nilihamia kwa bosi mwingine anaitwa Magibu aliyekuwa na magari yanayofanya kazi safari zake kutoka Arusha kwenda Kahama na muda mwingine yanakwenda Tabora,” anasema.

MITIHANI INAANZA

Shomari anasema kazi ya magari ina mitihani mingi, lakini hawezi kusahau tukio la kuharibikiwa na gari porini na kutojulikana mahali alipo kwa kukosekana kwa mawasiliano.

“Enzi hizo simu hazikuwapo kama ilivyo sasa, ilikuwa shida kupata mawasiliano ya haraka, ila nakumbuka wakati ninasafiri, gari letu likatuharibikia njiani kwa siku tatu watu hawajui tupo wapi,” anasema.

Anasema baada ya gari lao kutengemaa waliendelea na safari, lakini ile wanafika Arusha akapewa taarifa kwamba mdogo wake amefariki na alishazikwa nyumbani kwao jijini Tanga.

“Jambo hili liliniumiza sana, mpaka leo huwa naumia kushindwa kumzika mdogo wangu, lakini ndio maisha na mitihani yake,” anasema.

MIAKA MINGI YA USUKA

Shomari anasema alidumu kwenye kazi ya udereva kwa kipindi cha miaka 18 tangu mwaka 1990 mpaka 2008, tatizo la macho lilipomuanza kama utani na kumtesa kabla ya kupofuka kabisa.

Anasema lau kama sio tatizo hilo la macho huenda mpaka sasa labda angekuwa akiendelea na shughuli hiyo na pengine angekuwa mbali zaidi kimaisha kwani, ni moja ya kazi iliyokuwa ikimwingizia kipato chake na kuipenda kwa dhati.

CHANZO CHA UPOFU

Anasema mara ya mwisho kushika usukani ilikuwa kipindi akiendesha magari ya Kampuni ya Mtei yanayotoka Arusha kwenda Babati, kutokana na kuaminika sana na bosi wake alikuwa akipendwa sana.

Anasema tatizo lake la macho lilianza rasmi mwaka 2006, anasema ghafla tu macho yake yalikuwa kama yakipata ukungu na kuona kwa shida, ila akaendelea kukomaa na usukani kiubishi huku akiamini ipo siku mambo yatakuwa safi.

Anadai alikuwa anahofia kupoteza kazi aliyopewa na huku akiaminiwa mno na bosi wake, hivyo akaendelea kupiga mzigo huku macho yakiendelea kumsumbua.

“Sikuwahi kuwa na historia ya kuumwa macho katika maisha yangu, wala sijawahi hata kuvaa miwani eti kwa sababu ya macho, lakini hali ilipozidi kuwa mbaya niliamua kunyoosha mikono juu kwa kuhofia kuja kusababisha ajali barabarani.”

Anasema alikuwa akiona maluweluwe kila anapokuwa nyuma ya usukani, kitu kilichompa shida sana, kwani alipokuwa nje ya gari macho yalikuwa ya kawaida.

“Kitu kilichostaajabisha ni kwamba, macho yalikuwa hayawashi wala kuuma, ila nilikuwa naona vitu kama moshi vile kwa muda mrefu, ndipo nikaenda Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru nikapewa dawa za kutumia, ila hali haikubalika.”

“Kuna wakati niliishiwa pozi maana daktari aliniambia nina ugonjwa wa trakoma nikaona kama anayenizingua, hivyo nikahamia katika hospitali nyingine. “Nilienda Hospitari ya St Elizabeth (Kwa Babu), maarufu sana eneo la Levolosi. Nakumbuka ilikuwa mwaka 2008 na kukutana na daktari wa macho ambaye alinipima na kunipa dawa,” anasema na kuongeza;

“Daktari huyo aliniambia nikae kwa muda wa wiki moja nikiendelea kutumia dawa alizonipa kisha nirejee tena kwa vipimo zaidi, sikuwa na jinsi nilifanya kama nilivyoagizwa.”

Unajua alivyorejea hospitalini hapo kuchukuliwa vipimo zaidi, aligundulika ana tatizo gani?

Kabla ya kuhamia katika udereva uliomsababishia matatizo hayo ya macho, Allan Shomari beki wa kati alifanya mambo gani kwenye soka la Tanzania na amewahi kukumbana na mikasa ya aina gani?

Ungana na mwandishi wa makala haya katika toleo la Jumanne ijayo upate undani zaidi.