LAWRENCE : Dogo wa tasnia ya filamu anayekimbiza wakongwe

Saturday January 28 2017Jenifer Lawrence

Jenifer Lawrence 

KIUMRI bado mdogo, ana miaka 26 lakini Jennifer Lawrence tayari ameonyesha umahiri katika kuigiza filamu za kuvutia na ambazo zimempa utajiri huku akiwaacha mbali wakongwe wa tasnia hiyo.

Kwa mwaka wa pili mfululizo, 2015 na 2016, jina lake limekuwa katika nafasi ya kwanza kwenye orodha ya waigiza filamu wanawake waliotengeneza fedha nyingi kwa miaka hiyo.

Mara yake ya kwanza kuingia katika orodha ya Forbes ya matajiri waigiza filamu wanawake ilikuwa 2014 aliposhika nafasi ya pili na baada ya hapo akawa wa kwanza mara mbili.

Mwaka 2016, ametengeneza Dola 46 milioni kabla ya kodi wakati aliyeshika nafasi ya pili, Melissa McCarthy ametengeneza Dola 33 milioni akiwa amemzidi kwa tofauti kubwa, Dola 13 milioni.

Mafanikio ya Jennifer kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na mfululizo wa filamu za Hunger Games zilizotengeneza fedha nyingi, lakini kwa jumla ni kama ameanguka kwa mwaka 2016 ukilinganisha na mwaka 2015.

Mwaka 2015 alitengeneza Dola 52 milioni, ukilinganisha na pato la mwaka huu ukweli ni kwamba, msanii huyo ameanguka ingawa ni mshindi na anabaki kuwa bora miongoni mwa waigizaji filamu wanawake duniani. Jennifer alizaliwa Agosti 15, 1990, California, Marekani, utotoni mama yake alichukua uamuzi wa ajabu, alimkataza kucheza na watoto wa kike wenzake, aliamini kufanya hivyo kutamfanya awe mpambanaji lakini pia utundu wa mtoto huyo nao unadaiwa kumfanya mama yake achukue uamuzi huo.

Jennifer mwenyewe pia hakujiona mwenye kufaa kujumuika na wasichana wenzake shuleni hali hiyo ilizidi baada ya kuanza kupanda jukwaani kufanya maonyesho hasa maigizo yaliyomfanya kujiamini na kujijengea dhana kwamba kuna siku angefanikiwa.

Mbali na uigizaji akiwa shule pia alipenda kucheza mpira wa magongo na kikapu, ajabu ni kuwa alipenda kucheza katika timu ya wavulana ambayo pia baba yake alikuwa akiifundisha.

Jeninifer ambaye pia alipenda michezo ya kukimbia na farasi, alipenda kumwambia baba yake kwamba anajua kuna siku atakuwa staa huku akimhadithia baadhi ya michezo ya maigizo aliyoshiriki.

Akiwa na miaka tisa alishiriki mchezo wa kuigiza na kujipa jukumu la mwanamke malaya katika kanisa, mafanikio yake katika igizo hilo yalimfanya apongezwe na ndugu zake na huo ukawa mwanzo mzuri wa kujikita katika tasnia ya filamu.

Alianza kuigiza filamu kibiashara mwaka 2006 akiwa na Kampuni ya Town, alishiriki katika simulizi kadhaa za televisheni ikiwamo Monk mwaka 2006 na Medium mwaka 2007 na mwaka 2009 mafanikio yake yalimpa tuzo ya Young Artist.

Jennifer pia tayari ametengeneza filamu ya Mother ambayo inawahusu wapenzi wawili ambao maisha yao yalivurugika baada ya kupata wageni ambao hawakuwatarajia na inatarajia kutolewa mwaka huu. Mwaka 2010 wakati akitengeneza filamu ya X-Men: First Class, Jennifer aliingia katika mahusiano ya kimapenzi na mwigizaji mwenzake, Nicholas Hoult ingawa walitibuana na kuachana mwaka 2013.

Ni kipindi hicho hicho ndipo picha za utupu za Jennifer zilipozagaa kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, mwenyewe aliibuka akidai kuwa picha hizo hazikutakiwa kuonekana na mtu yeyote aliyeziona alifanya kosa la jinai katika mahusiano, aliingilia uhuru wa mtu binafsi na kwamba mtu huyo au watu hao wanatakiwa kuona aibu kwa kosa hilo.