Yaya Toure Mwanasoka Bora wa Mwaka Afrika

Saturday January 11 2014

 

LAGOS, NIGERIA

KIUNGO, Yaya Toure, amechaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Afrika ikiibuka kwa mara ya tatu mfululizo na kuwabwaga mastaa kadhaa akiwamo Mnigeria, John Obi Mikel.

Kwenye tuzo zilizofanyika mjini Lagos, Nigeria juzi Alhamisi usiku, kiungo huyo wa Manchester City alimpiku staa mwenzake pia wa Ivory Coast, straika, Didier Drogba.

Kwa kutwaa tuzo kwa miaka mitatu mfululizo, jambo hilo limemfanya Toure, 30, kufikia rekodi za Abedi Pele na Samuel Eto’o waliowahi kufanya hivyo huko nyuma.

Mikel ameshindwa kumshinda Yaya Toure na kuifariji Nigeria ambayo mara ya mwisho kwa nyota wake kutwaa tuzo hiyo ilikuwa mwaka 1999 wakati fowadi, Nwankwo Kanu, alipoibuka kidedea.

Yaya Toure alikuwa mchezaji muhimu wa Ivory Coast wakati walipotinga robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana na mbio za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil mwaka huu, lakini Mikel alikuwa akipewa nafasi pia kutokana na kuisaidia Nigeria kutwaa ubingwa wa Afrika na kufuzu Kombe la Dunia.

Tuzo nyingine zilitolewa kwa Stephen Keshi (Kocha Bora) na kiungo wa Misri, Mohamed Aboutrika (Mwanasoka Bora wa Soka la Ndani)  huku tuzo ya gwiji la Afrika ikinyakuliwa na kocha, Bruno Metsu, ambaye kwa sasa ni marehemu.