Wenger ajishangaa kwa ubahili

Kocha  Arsene Wenger.

Muktasari:

  • Kocha huyo Mfaransa amedai pia hapendi kutumia pesa nyingi kwenye usajili kwa sababu anaogopa kufanya makosa ya kuitia hasara timu. Mashabiki wa Arsenal walikuwa wakiimba nyimbo za kumtaka kocha huyo atumie pesa kusajili baada ya mechi yao ya sare ya bila kufungana dhidi ya Leicester City, ambapo staa wao mpya Ahmed Musa, aliyeingia kutokea benchi aliwapa wakati mgumu

London,England. HATIMAYE Kocha bahili Arsene Wenger ameshtuka. Kocha huyo wa Arsenal amekiri kwamba anajishangaa kuona kwa nini anaona uchungu kutumia pesa za timu hiyo kwenye usajili utadhani zinatoka mfukoni mwake.

Kocha huyo Mfaransa amedai pia hapendi kutumia pesa nyingi kwenye usajili kwa sababu anaogopa kufanya makosa ya kuitia hasara timu. Mashabiki wa Arsenal walikuwa wakiimba nyimbo za kumtaka kocha huyo atumie pesa kusajili baada ya mechi yao ya sare ya bila kufungana dhidi ya Leicester City, ambapo staa wao mpya Ahmed Musa, aliyeingia kutokea benchi aliwapa wakati mgumu.

Mashabiki hao wa Arsenal kwa muda sasa wamekuwa wakimshutumu Wenger kwa kitendo chake cha kufanyia ubahili na uvivu wa kutumia pesa za klabu utadhani ni zake. Baada ya kushindwa kufanya usajili wowote wa maana na kuona nafasi yao kwenye Top Four ikiwa kwenye mushkeli mkubwa msimu huu, Mfaransa huyo sasa amekiri kuwa yeye ni bahili.

Kwenye kitabu cha Alan Curbishley, Game Shangers: Inside English Football, Kocha Wenger, 66, alisema: “Binafsi nadhani njia pekee ya kuwa kocha mzuri ni kutumia pesa za klabu kama unavyotumia pesa zako, kwa sababu kama hutofanya hivyo, basi unafanya makosa makubwa.

“Unafanya uamuzi na nadhani ni vyema utumie kama unavyofanya pesa zako, utumie pesa tu kama wewe ndiye mmiliki wa klabu, kwa sababu usipofanya hivyo, hufiki mbali.” Wenger amefanya usajili mmoja tu wa pesa nyingi msimu huu baada ya kutumia Pauni 30 milioni kumnasa kiungo wa Uswisi, Granit Xhaka na bado anasuasua kutumia pesa nyingi kwa beki wa kati Shkodran Mustafi na straika Alexandre Lacazette. Wakati akiona Mustafi ada yake ya Pauni 50 milioni ni kubwa, West Brom wamemwambia pia beki wao Jonny Evans anapatikana kwa Pauni 25 milioni.