SING'OKI: Mourinho asema mtangoja sana

Monday November 2 2015

 

LONDON, ENGLAND

KUNA watu wana utani sana. Unajua wanasema nini? Eti viganja vya Jose Mourinho kwa sasa vimelowa jasho akiwa ameshika simu yake kwa hofu ya meseji na simu zinazoingia kwa sasa mojawapo isiwe ya namba ya Bilionea Roman Abramovich.

Taarifa za kutoka Ureno zinadai kwamba muda wowote anaweza kupokea meseji kutoka kwa bosi huyo bilionea mmiliki wa klabu ya Chelsea baada ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England kufanya vibaya kwenye ligi msimu huu.

Mourinho yupo kwenye hatari ya kufutwa kazi klabuni Chelsea kwa sasa. Kocha huyo na benchi lake lote la ufundi walifahamu wazi kwamba wanakwenda kumenyana na Liverpool juzi Jumamosi wakiwa na kazi moja tu, kushinda kinyume na hilo, basi kibarua kipo hatarini.  Hata hivyo, mwenyewe amesema hang’oki, licha ya mara ya kwanza alipohojiwa na waandishi, aligoma kuzungumza.

Chelsea imekumbana na kipigo cha mabao 3-1 na kilichobaki kwa sasa ni mmiliki tu, Abramovich kuchukua hatua.

Taarifa kutoka Ureno zinadai kwamba wanaamini Mourinho hatakuwapo kwenye benchi la timu hiyo itakapomenyana na Dynamo Kiev kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano hii.

Mourinho alisaini mkataba mpya wa miaka minne Agosti mwaka huu na anapokea mshahara wa Pauni 9.5 milioni kwa mwaka.

Mkataba huo umeelezwa kwamba kuna kipengele kinachofichua kwamba atalipwa mshahara wa mwaka mmoja kama mkataba wake utasitishwa.

Kichapo hicho cha juzi ni cha sita kwa Chelsea katika mechi 11 za Ligi Kuu England msimu huu na hivyo timu inaendelea kushika namba 15 kwenye msimamo wa ligi, huku Mourinho akiendelea kutoa lawama zake kwa marefa.

Alisema: “Tulishinda 1-0 na kuliongezwa dakika mbili za majeruhi. Lakini, tulifungwa bao baada ya dakika mbili na sekunde 35 za muda huo wa majeruhi katika kipindi cha kwanza na kilichotokea kipindi cha pili ni mwendelezo ule wa kipindi cha kwanza.”

Maofisa wa Chelsea juzi usiku walisisitiza kwamba Mourinho hajafutwa kazi na walisema kwamba hakukuwa na kikao chochote na mmiliki Abramovich. Hata hivyo, kumekuwa na imani kubwa kwamba kibarua cha Mourinho kinaweza kufutika muda wowote kutoka sasa kutokana na hali ya mambo ilivyo.

Mourinho aliulizwa juzi baada ya mechi hiyo ya kipigo kwamba ni ya mwisho kwake kubaki Chelsea, alijibu: “Hapana, siondoki.” Aliongeza: “Sina wasiwasi, sina wasiwasi kabisa.

Wachezaji hawapewi heshima yao inayostahili.”

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema anamwonea huruma Mourinho kwa kuwa hali aliyonayo ni kama ile aliyowahi kuwa nayo mwaka jana alipokuwa na Dortmund.