Pogba ataka achezeshwe mshambuliaji

KIUNGO Paul Pogba amemwambia kocha wake, Jose Mourinho aanze kumpanga kwenye safu ya ushambuliaji kikosini Manchester United.

Staa huyo aliyenaswa kwa Pauni 89 milioni na kuweka rekodi ya dunia kwenye uhamisho amekuwa akitumiwa zaidi kwenye nafasi ya kiungo wa kukaba tofauti na anavyotumika kwenye kikosi cha Ufaransa.

Alipotumiwa kwenye eneo la kushambulia zaidi, Pogba alifunga bao maridadi kwa shuti la mbali wakati Ufaransa ilipoichapa Uholanzi 1-0 kwenye kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2018.

Kwenye kikosi cha Man United, Mourinho amempanga Pogba kwenye sehemu ya kiungo kitu ambacho kinamnyima nafasi ya kuonyesha makali yake katika kuisaidia timu.

Pogba alisema: “Najaribu kuzoea nafasi hii. Mimi ni mchezaji ninayependa kwenda mbele zaidi.

“Kocha amenipa maagizo, najaribu kuyafuata. Lazima ninyang’anye mipira na kuweka mkazo zaidi kwenye kulinda. Inanipa wakati mgumu kiasi fulani kwenye kucheza, kwa sababu nataka kucheza mpira kwenda mbele.”