Pauni 220,000kwa wiki kumshusha Griezmann Trafford

Saturday January 7 2017

 

PESA ina nguvu asikwambie mtu. Na ndio maana Jose Mourinho anaifanya kuwa silaha yake kikosini Manchester United.

Kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi alitumia pesa kumnasa Paul Pogba, pesa ambayo isingekuwa rahisi kuzuia dili hilo lisifanyike.

Real Madrid nayo ilikuwa ikimtaka Pogba, lakini Man United baada ya kuweka mezani pesa ya maana, akakubali kurejea Old Trafford kwa ada ya uhamisho ambayo inaweka rekodi ya dunia ya Pauni 89 milioni.

kwa sasa Mourinho anaingia tena sokoni kusaka jembe la maana. Anamtaka supastaa wa Ufaransa na Atletico Madrid, Antoine Griezmann. Vita ya kumnasa staa huyo si ndogo baada ya Kocha, Arsene Wenger wa kikosi cha Arsenal, naye kuhitaji saini ya Mfaransa mwenzake huyo atue Emirates.

Lakini, Mourinho amemwambia Griezmann kwamba, atalipwa mshahara mkubwa kama wa mastaa wengine Old Trafford akiwano Pogba kama tu atakubali kutua kuichezea Man United. Ripoti za kutoka Old Trafford zinafichua kwamba, mabosi wa timu hiyo kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na wawakilishi wa Griezmann wakizungumzia maslahi binafsi kabla ya kwenda kumalizana na Atletico ili wamchukue staa wao.

Mabosi wa Man United wamemwambia Griezmann, 25, itamlipa mshahara wa Pauni 220,000 kwa wiki kama anavyolipwa Pogba, pamoja na bonasi zilezile anazolipwa mwanasoka huyo ghali duniani ili kuhakikisha anatua kwenye kikosi chake. Pogba na Griezmann ni marafiki wakubwa na Man United inataka kutumia kigezo hicho ili kuinasa saini yake.

Tangu mwaka jana, Man United imemweka Griezmann kwenye orodha ya washambuliaji namba moja kabisa inayowataka kuwaongeza kwenye kikosi chake ili kukifanya kuwa na makali ya kutisha kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Inachokifanya United kwa sasa ni kuafikiana makubaliano binafsi na mchezaji huyo kabla ya kuigeukia Atletico Madrid, ambapo inaamini haitakuwa na mahitaji makubwa zaidi ya Pauni 86 milioni zilizoandikwa kwenye mkataba wake.

Kwenye mpango huo, Man United imepanga kuishawishi Atletico kumjumuisha mchezaji mmoja katika dili hilo ili kuwafanya wababe hao wa La Liga wasifikirie sana machungu ya kumpoteza mkali wao kwa sababu watakuwa wamevuna pesa pamoja na mchezaji huyo.

Mourinho anataka kukamilisha dili hilo kwenye dirisha hili la uhamisho wa Januari, japo inawezekana kuwa vigumu kwa sababu Atletico itahitaji kubaki na silaha yake hiyo kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo, sasa imeingia kwenye hatua ya mtoano ya 16 bora itakayoendelea mwezi ujao.

Pogba amesaini mkataba wa miaka minne wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi huku akiwa na haki ya malipo yanayohusu taswira zake ukiweka kando mshahara anaovuta kila wiki.

Atalipwa Pauni 5 milioni isiyokatwa kodi kama bonasi endapo ataendelea kubaki Old Trafford kwa kipindi cha miaka miezi. Ofa zote hizo alizopewa Pogba, Man United imemwambia Griezmann naye atafanyiwa vivyo hivyo, kitu cha kufanya ni kuchagua tu kutua Old Trafford.