Mourinho aweka benchi ghali duniani

Muktasari:

Katika Uwanja wa Ewood Park ambako United ilishinda mabao 2-1 na kutinga hatua ya robo fainali, iliweka rekodi ya kuweka benchi ghali zaidi katika historia ya michuano hiyo.

HATA kama nafasi ya sita imewang’ang’ania lakini jeuri ya pesa bado Manchester United. Juzi imeonyesha jeuri ilipoitoa Blackburn katika FA.

Katika Uwanja wa Ewood Park ambako United ilishinda mabao 2-1 na kutinga hatua ya robo fainali, iliweka rekodi ya kuweka benchi ghali zaidi katika historia ya michuano hiyo.

Jumla mastaa saba wa United walikaa katika benchi ambapo wachezaji hao wameigharimu United dau la Pauni 192 milioni wakiongozwa na staa kiungo, Paul Pogba ambaye ilimnunua Agosti mwaka jana kwa dau la Pauni 89 milioni kutoka Juventus na kuvunja rekodi ya dunia.

Katika benchi hilo mchezaji aliyefuatia kwa gharama alikuwa kiungo, Juan Mata ambaye United ilimnunua kwa dau la Pauni 37 milioni Januari 2014 kutoa Chelsea ambayo wakati huo ilikuwa inafundishwa na Mourinho.

Katika benchi hilo pia alikuwepo beki wa kushoto, Luke Shaw ambaye amekuwa akisuasua katika utawala wa Mourinho. Shaw alinunuliwa kutoka Southampton Julai 2014 kwa dau la Pauni 30 milioni.

Mwingine aliyekuwa katika benchi hilo na ambaye alikuwa amenunuliwa kwa dau kama la Shaw ni beki wa kati wa kimataifa wa Ivory Coast, Eric Bailly ambaye alikuwa mchezaji wa kwanza kununuliwa katika utawala wa Mourinho akigharimu dau la Pauni 30 milioni kutoa Villarreal.

Aliyekamilisha dau la Pauni 192 milioni alikuwa kiungo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani, Bastian Schweinsteiger aliyenunuliwa kutoka Bayern Munich kwa dau la Pauni 6.5 milioni wakati wa utawala wa kocha aliyepita kabla ya Mourinho, Louis van Gaal.

Hata hivyo, katika benchi hilo kulikuwa na wachezaji wawili ambao hawakuigharimu United kiasi chochote cha pesa. Wa kwanza alikuwa staa, Zlatan Ibrahimovic ambaye licha ya mshahara wake mkubwa wa Pauni 200,000 kwa wiki pale Old Trafford, lakini alichukuliwa bure kutoka PSG kwa sababu alikuwa amemaliza mkataba.

Kukamilisha benchi hilo alikuwepo kinda, Dean Henderson ambaye ni kipa wa timu ya vijana ambaye alikuwa akisubiri nafasi yake kama kipa Sergio Romero angeumia katika pambano hilo.

Henderson hajaighatimu kitu United.