Mourihho achonga usiku mzima

JOSE MOURINHO

Muktasari:

MATAJI TU

Jose Mourinho ameongeza katika kabati taji la tatu akiwa na Man United, baada ya kuanza na Ngao ya Hisani, Kombe la Ligi na sasa amebeba la Europa.

STOCKHOLM, SWEDEN. KOMBE lipo kabatini na sasa ni zamu ya Jose Mourinho kuchonga. Juzi katika Jiji la Stockholm, Mourinho ameongea mengi baada ya Man United kufanikiwa kuichapa Ajax na kutwaa ubingwa wa Europa ambao, unawapa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Mabao mawili ya Paul Pogba na Henrikh Mkhitryan yalitosha kabisa kumwongezea Mourinho taji katika msimu huu, lakini mwenyewe anadai huu ulikuwa msimu mgumu kuliko yote aliyowahi kushiriki katika soka.

Sasa Mour inho ame maliza msimu akiwa ametwaa Ngao ya Jamii, Kombe la Ligi na ubingwa wa Europa ingawa mwenyewe anadai kwamba, haukuwa msimu rahisi kabisa kwake.

“Mataji matatu katika msimu mmoja pamoja na nafasi ya Ligi ya Mabingwa. Nina furaha sana kwa sababu huu ndio ulikuwa msimu mgumu zaidi nikiwa kama kocha. Ni mwisho wa msimu mgumu lakini umekuwa msimu mzuri sana,” alisema Mourinho.

Katika pambano la juzi, Man United walimiliki mpira kwa asilimia 31 tu huku Ajax wakimiliki zaidi, lakini huku wakishindwa kutengeneza nafasi za kufunga na katika mashuti 17 ambayo walipiga katika lango la kipa, Sergio Romero ni mashuti matatu tu ndiyo yaliyolenga lango.

Kwa upande wa Man United wao walipiga mashuti saba katika lango la Ajax ambalo lilikaliwa na kipa wa kimataifa wa Cameroon, Andre Onana na manne kati ya hayo yalilenga lango na mawili kuzalisha mabao hayo.

Pamoja na takwimu hizo, Mourinho amedai alipagwa na kikosi chake kilivyocheza huku akidai urembo wa soka hauleti mataji.

“Kama ukitawala katika mipira ya juu unafika haraka. Kuna urembo mwingi lakini huwa haushindi mataji. Tulijua sisi tulikuwa bora kuliko wao na tulitumia mapungufu yao. Tulipendelea kufika katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kupitia njia hii kuliko kushika nafasi ya nne, tatu au ya pili,” alitamba Mreno huyo.

“Tumefikia malengo yetu, tumefika Ligi ya Mabingwa kwa kushinda taji, taji muhimu. Sasa klabu hii ina kila taji duniani. Tulipambana sana tangu mwanzo. Siku zote tuliamini tungetwaa kombe la Europa na sasa tuna furaha. Tulicheza kwa akili na tulishinda kwa raha kabisa,” alisema.

Wakati Mourinho akijitamba, Kocha wa Ajax, Peter Bosz aliiponda staili ya soka ya Man United huku akidai iliifanya Ajax iwe katika wakati mgumu kucheza katika staili yao ambayo wameizoea na hakuona ubora wowote kutoka kwa timu zote mbili.

“Kukabia juu ilikuwa shida kwa sababu Man walicheza mipira mirefu tu na hawakutaka kujihatarisha kabisa kwa kupanga mashambulizi kuanzia nyuma. Nadhani mechi iliboa. Hakukuwa na nafasi zozote kwa pande zote mbili,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi.

“Nimekerwa kwa sababu unacheza fainali ili kushinda ila hatukishinda Sijaiona soka la uhakika,” alisema.

Kwa mfumo mpya wa Ligi ya mabingwa ni Chelsea tu ndio timu ya Kiingereza ambayo itapewa nafasi ya kuongoza kundi lao huku United wakipewa nafasi ya pili katika kundi ambapo watakuwa katika mkumbo mmoja wa nafasi hiyo na timu kama Barcelona, Atletico Madrid, PSG, Borussia Dortmund, Man City na Porto na kuzikimbia timu za Real Madrid, Juventus, Monaco, Bayern Munich.