Messi atengeneza pengo Barca

BARCELONA, HISPANIA

BARCELONA imepata pigo, MSN imetibuka. Usijiulize, MSN ni kifupi tu majina ya mastaa wanaounda safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ya Barcelona, yaani Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar, kiboko ya mabao. Lakini, sasa imetibuka.

Ni hivi, safu hiyo sasa itamkosa staa wake Messi kwa kipindi kisichopungua wiki tatu baada ya fowadi huyo wa kimataifa wa Argentina kupata maumivu katika sare ya 1-1 kwenye La Liga dhidi ya Atletico Madrid juzi Jumatano.

Staa huyo aligongana na beki wa Atletico, Diego Godin na alipata maumivu kwenye mguu wake wa kulia.

Hata hivyo, tatizo hilo lililompata Messi limeripotiwa kuwa ni la siku nyingi ambapo aliwahi kukumbana nalo kwenye mechi za kimataifa na sasa kuna wasiwasi akakosa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Monchengladbach.

Mechi nyingine atakazokosa staa huyo ni pamoja na Sporting Gijon na Celta Vigo na atahitajika kupambana sana na majeraha hayo kuweza kuikabili Manchester City kwenye Uwanja wa Camp Nou mwishoni mwa Oktoba.

“Kumpoteza Messi kuna maana soka limepotea. Tukiwa na Messi tunakuwa na nguvu, lakini tutajaribu kupambana kwa nguvu zote,” alisema Kocha wa Barcelona, Luis Enrique.