Ghana yadaiwa kuhonga waamuzi

GYAN

ACCRA, GHANA

SHIRIKISHO la Soka la Ghana limekanusha kuhusiana na ripoti kutoka kwenye moja ya magazeti ya nchi hiyo kwamba waliwahonga waamuzi katika mechi zao za kufuzu Kombe la Dunia 2014.

Gazeti hilo la michezo la Ghana lilitoka na ripoti mapema wiki hii kwamba Black Stars ilitumia Dola 720,000 kuwahonga waamuzi waliochezesha mechi zao za kufuzu Kombe la Dunia 2014, fainali ambazo zilifanyika nchini Brazil.

Dola 16,000 zilitumika kwenye mechi ya mchujo dhidi ya Misri, ambapo Black Stars ilishinda jumla ya mabao 7-3, kufuatia ushindi wa 6-1 kwenye mechi iliyofanyikwa kwao.

Shirikisho hilo la soka la Ghana limekana vikali kuhusu ripoti hiyo na sasa wanafikiria kwenda mahakamani.

Mmoja wa mastaa wa Ghana waliokuwa kwenye kikosi hicho ni Asamoah Gyan.

Taarifa ya shirikisho hilo ilibainisha: “Chama cha soka Ghana (GFA) kimetambua kuwapo na gazeti moja la michezo tolea la Jumatatu, Julai 18, 2016 kwamba kuna habari inayoeleza Ghana tulihonga ili kufuzu Kombe la Dunia 2014.

Ni uongo, hatukuwa na bajeti ya kuhonga wala kufanya vitu vingine vya kijinga namna hiyo.”