EPL kubwa

Muktasari:

  • “Kuna klabu ambayo inachokijua ni kutumia tu pesa kusajili wachezaji mashuhuri. Mimi nataka kuwa tofauti. Nadhani ningekuwa tofauti pia kama ningekuwa natumia pesa nyingi kusajili.”

LONDON, ENGLAND

NDANI ya uwanja, mastaa wa Liverpool wamekimbia kilomita nyingi kwenye Ligi Kuu England kuliko mastaa wa Manchester United na nyota hao watamaliza ubishi wa nani noma na nani dhaifu keshokutwa Jumatatu.

Hadi kufika sasa wakati ligi hiyo ikiwa imechezwa mechi saba kwa kila timu, mastaa wa Liverpool wamekimbia kilomita 815 ndani ya uwanja, wakati Man United wao wamekimbia kilomita 736.

Mambo ya uwanjani, yamewafanya makocha wa timu hizo mbili, Jurgen Klopp wa Liverpool na Jose Mourinho wa Man United kupigana vijembe kuhusu wachezaji, Klopp akisema: “Kuna klabu ambayo inachokijua ni kutumia tu pesa kusajili wachezaji mashuhuri. Mimi nataka kuwa tofauti. Nadhani ningekuwa tofauti pia kama ningekuwa natumia pesa nyingi kusajili.”

Mourinho akamjibu: “Ninaposikia maneno ya makocha wanakosoa matumizi ya pesa, sioni kama ni tatizo lao, tatizo ni kwamba unahitaji kuwapo kwenye klabu ya daraja la juu duniani. Ukiwa Man United vitu kama hiyo ni kawaida.”

Ubishi wa makocha hao utamaliza Jumatatu kwenye Uwanja wa Anfield, ambapo vita kubwa kwenye sehemu ya kiungo itatarajiwa kati ya Jordan Henderson dhidi ya Paul Pogba, huku Liverpool ikiwa kwenye presha ya kuwakosa mastaa wake Adam Lallana, Georginio Wijnaldum, Dejan Lovren na Nathaniel Clyne, ambapo wapo kwenye hatihati ya kucheza mechi hiyo. Lakini, jambo zuri analofurahia Klopp ni fowadi yake yote, Philippe Coutinho, Roberto Firmino, Sadio Mane na Daniel Sturridge wote kuwa fiti, nakwambia Man United wataipatapata. Ni ubabe ubabe tu.

Wakati ikisubiriwa kipute hicho cha Jumatatu, utamu wa Ligi Kuu England utaanzia leo Jumamosi ambapo mchana kweupe, Chelsea itakuwa Stamford Bridge kucheza na Leicester City, moja ya mechi ngumu kabisa katika wikiendi hii. Chelsea watashuka uwanjani kucheza mechi hiyo wakiwa kwenye presha kubwa baada ya kupoteza mechi mbili msimu huu kwenye ligi. Arsenal ambao hawajapoteza mechi yoyote tangu walipofungwa na Liverpool mwanzoni mwa msimu wao, wao watakuwa na kazi nyepesi tu nyumbani Emirates watakapomenyana na Swansea City, ambao hivi karibuni walitimua kocha wao na Arsene Wenger anataka kutumia nafasi hiyo kujiimarisha zaidi kileleni. Manchester City, ambao wanauguza maumivu ya kupigwa mechi iliyopita, watakuwa Etihad kukipiga na Everton, wakati Bournemouth watakipiga na Hull City nyumbani na Stoke City mdogo mdogo baada ya kupata sare kwa Man United wiki mbili zilizopita itakipiga na Sunderland.

West Brom wao watakuwa nyumbani kuikaribisha Tottenham Hotspur na Crystal Palace watakuwa na kazi mbele ya West Ham United, wakati kesho Jumapili, Middlesbrough watawakaribisha Watford na Southampton watamaliza ubishi na Burnley.