Chelsea kimenuka

Kocha wa Chelsea, Conte

Muktasari:

Walipochapwa 2-1 na Liverpool, usiku huo wa mechi bilionea huyo aliliweka kitimoto benchi la ufundi kwa nini wamechapwa mechi hiyo. 

KUWA kocha wa Chelsea ujipange, kazi sana asikwambie mtu. Shida ni bilionea mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich.

Walipochapwa 2-1 na Liverpool, usiku huo wa mechi bilionea huyo aliliweka kitimoto benchi la ufundi kwa nini wamechapwa mechi hiyo. Wakati Kocha Antonio Conte akijipanga kuhusu jambo hilo, kikosi chake kimekumbana na kichapo kingine, tena safari hii dhidi ya mahasimu wao wa kutoka jiji moja la London. Wamechapwa 3-0 na Arsenal na kuibua mjadala kwamba Abramovich huenda akaitisha kikao na bodi nzima.

Kuona kwamba kibarua chake kinaweza kuota mbawa kabla hata hajakifaidi vizuri, Kocha Conte sasa amefikiria kuwapiga chini mabeki wote waliocheza mechi hiyo ya Arsenal na kuruhusu mabao ya kijinga. Mabeki Branislav Ivanovic na Gary Cahill walihusika kwenye bao la kwanza la Arsenal kwa kufanya uzembe, lakini beki yao iliendelea kufanya makosa ambayo yameifanya hadi sasa kuruhusu mabao 12 kwenye wavu wao.

Kitu ambacho Conte anachosubiri ni mabeki wake wengine wa kati John Terry na Kurt Zouma wapone na wakiwa fiti tu, moja kwa moja wanakuja kikosi na jambo hilo litawagharimu waliocheza kizembe kwenye kipigo cha Arsenal. Conte anafikiria pia kumpiga chini beki wake mpya, Mbrazili David Luiz kutoka kwenye orodha ya mabeki wake wa kati chaguo la kwanza na ikifika Januari tu shughuli ya kwanza itakayofanyika ni kuhakikisha anawanasa Leonardo Bonucci na Kalidou Koulibaly.

Beki mpya, Marcos Alonso ameonyesha kiwango kizuri kwa dakika chache alizocheza na huenda panga hilo lisipite kwenye jina lake.

Ukiwaweka kando mabeki hao, Conte anawafikiria pia Michael Keane na Ben Gibson ambapo amewatuma skauti wake kuhakikisha wanawafuatilia kwa karibu wachezaji hao ili kuona kama wataweza kufiti kwenye kikosi chake ili kuondokana na shida ya kuruhusu mabao ya kijinga.

“Unauliza nilichukia kipindi cha kwanza? Jibu langu ni ndio, lakini huwa napenda kutozungumza sana, kwa sababu ninafahamu kitu ambacho napaswa kukizungumza, nitazungumza na wachezaji wangu kuwaeleza ukweli,” alisema Conte.

“Ni kawaida. Kweli nilikasirika, lakini wachezaji wangu walikasirika pia. Hii ni kwa sababu hatukufurahishwa na mchezo wetu na kiwango chetu. Sikulala, sikulala kabisa.”

Kwenye orodha ya mabeki wa Chelsea waliopo kwenye kikosi hicho cha Mtaliano Conte ni Cesar Azpilicueta, Cahill, Ivanovic, Terry, Luiz, Zouma, Ola Aina na Marcos Alonso.

Chelsea kwa sasa inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi zake 10, pointi nane pungufu ya kuwafikia vinara Manchester City, ambao wamekuwa na rekodi nzuri ya ushindi wa asilimia 100 tangu msimu huu uanze.

Nne Bora ya Ligi Kuu England kwa sasa inaundwa na Man City, Tottenham Hotspur, Arsenal na Liverpool, wakati vijana wa Jose Mourinho, Manchester United wanashika nafasi ya sita, huku Everton ya Ronald Koeman ipo kwenye nafasi ya nne.