BYE BYE: Joe Hart azua majonzi Man City

2006  Ni mwaka ambao Joe Hart alijiunga na Manchester City akitokea  Shrewsbury Town.  Amecheza jumla ya mechi  266.

Muktasari:

  • Tayari kipa Claudio Bravo ametua jijini Manchester kukamilisha uhamisho wa Pauni 17 milioni akitokea Barcelona huku Guardiola akimwona kuwa ndiye kipa mwafaka kwa staili yake ya kuchezesha timu kuanzia nyuma.

MAMBO hufika mwisho. Licha ya kuwa mchezaji anayeheshimika sana Etihad, lakini juzi Joe Hart amelazimika kuwaaga mashabiki wa timu hiyo huku akikaribia kutokwa na machozi baada ya kucheza pambano ambalo linasadikika kuwa la mwisho kwake klabuni hapo.

Kocha Pep Guardiola alimweka kipa huyo langoni katika pambano la kufuzu Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Steaua Bucharest lililopigwa Etihad juzi usiku huku pambano hilo kuonekana kutokuwa muhimu baada ya City kushinda 5-0 pambano la awali.

Tayari kipa Claudio Bravo ametua jijini Manchester kukamilisha uhamisho wa Pauni 17 milioni akitokea Barcelona huku Guardiola akimwona kuwa ndiye kipa mwafaka kwa staili yake ya kuchezesha timu kuanzia nyuma.

Hart alicheza pambano hilo akiaga na katika dakika ya 66 mashabiki wa timu hiyo walisimama uwanja mzima huku wakiimba wimbo ‘Kama unampenda Joe Hart simama na uimbe’.

“Ulikuwa usiku wa kipekee kwangu. Nimekuwa na usiku kadhaa katika soka lakini usiku huu ulikuwa mzuri sana kwangu. Wote tunajua kuwa kuna kitu kinaendelea lakini mimi ni mtu wa ndani humu na naona kuwa tunafanya vizuri kama timu na tuna menejimenti nzuri,” alisema Hart.

“Nina furaha sana na timu usiku wa leo. Ulikuwa usiku mzuri kwetu na hasa mimi. Hii ni sehemu maalumu kwangu na hakuna siri kwamba ni sehemu ambayo natamani niendelee kuwepo. Hata hivyo, kuna mambo huwa yanatokea katika soka lakini sisi ni wanaume na inabidi tusonge mbele, hata hivyo usiku wa leo ulikuwa mzuri. Nawashukuru watu wa Manchester City na nafurahi kwamba na wao wananikubali. Kwa hiyo ni hisia nzuri,” alisema Hart.

Hata hivyo, Kocha Guardiola alikiri kwamba alishamweleza wazi kipa huyo aliyenunuliwa kutoka Shrewsbury mwaka 2006 kuhusu maamuzi yake (ya kutomtumia tena)

“Najua ni mchezaji anayeheshimika hapa. Najua alivyo muhimu kwa klabu hii. Najua alichofanya kwa klabu hii. Ni sehemu ya historia. Akiwa na mataji ya Ligi Kuu na makombe, ni muhimu siyo tu kwa alichofanya uwanjani bali hata nje ya uwanja,” alisema Guardiola.

“Lakini anajua niliwasili na uamuzi wangu, pia ninachofikiria kuhusu nafasi yake. Nimefurahishwa na kiwango chake (dhidi ya Steaua) na ninapenda watu wanavyomsapoti na jinsi ilivyo muhimu kwake. Hakuna shaka kuhusu hilo,” alisema Guardiola.

Mashabiki wa City wameonekana kuchanganyikiwa kutokana na mapenzi makubwa waliyonayo kwa Hart, huku pia wakiwa na hamu kubwa ya kumwona Guardiola akikisuka kikosi chao na kuwa tishio barani Ulaya. Wanashindwa kumlaumu.

Hata hivyo, hatima ya Hart ipo shakani kwa kiasi kikubwa kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho. Kuna uwezekano mkubwa kipa huyo akadoda katika soka la uhamisho kutokana na mshahara mkubwa anaolipwa na Manchester City. Kipa huyo analipwa dau la Pauni 130,000 kwa wiki.

Awali ilitajwa kuwa Everton ilikuwa inataka kumchukua kipa huyo lakini mpaka sasa haijaonyesha nia madhubuti ya kumchukua. Kumekuwa na hisia pia kuwa kuna timu kama Celtic na Sunderland ambazo zinaweza kumtaka kwa mkopo kipa huyo lakini kama dili hilo likiwezekana, City watalazimika kuzisaidia kulipa mshahara wa kipa huyo.

Wakati wasiwasi huo ukiendelea, kuna mashaka kwamba kocha mpya wa England, Sam Allardayce atalazimika kumpiga chini katika kikosi chake kipa huyo kama akibaki Manchester City baada ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho Septemba Mosi mwaka huu.