BIFU KALI: Wakala wa Toure amjibu Guardiola kijeuri

Muktasari:

Awali, juzi mchana Pep alianza kwa kumtaka Seluk aombe msamaha kwa kauli nzito aliyotoa baada ya yeye kumuacha Yaya katika kikosi cha Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, lakini Seluk ameibuka na kudai Pep ndiye aombe msamaha kwa watu aliowakosea.

DAWA ya jeuri ni kiburi. Ndicho kinachoendelea kati ya Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola na wakala wa kiungo wa timu hiyo, Yaya Toure, Dimitri Seluk. Wapo katika bifu zito la kuvuana nguo, ambapo baada ya Pep kuanzisha vita, Seluk ameibuka ndani ya saa chache kujibu mapigo.

Awali, juzi mchana Pep alianza kwa kumtaka Seluk aombe msamaha kwa kauli nzito aliyotoa baada ya yeye kumuacha Yaya katika kikosi cha Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, lakini Seluk ameibuka na kudai Pep ndiye aombe msamaha kwa watu aliowakosea.

Seluk, amemtaka Guardiola awaombe msamaha Manuel Pellegrini ambaye anaamini alimzunguka katika kuchukua kiti chake, kisha amuombe msamaha kipa wa England, Joe Hart aliyemtimua bila ya heshima, kisha amuombe msamaha Yaya.

“Niombe msamaha kwa sababu gani?” alianza Seluk. Guardiola ameshinda mechi chache hapa anajiona yeye ni mfalme. Naishi Ulaya kwa hiyo naweza kusema ninachotaka na Guardiola hawezi kunizuia. “Sawa nitaomba msamaha kwa Guardiola kama na yeye akiomba msamaha kwa Pellegrini kwa kile alichomfanyia. Kama angekuwa muungwana jambo hilo halipaswi kutokea,” aliendelea Seluk.

“Pellegrini alisaini mkataba mpya mwaka jana halafu ghafla Guardiola akamuondoa. Pellegrini ni muungwana sana na Guardiola pia anahitaji kumuomba msamaha Hart. Sio kitu cha kawaida na sio haki kuja England na kuwafukuza wachezaji kadhaa wa Kiingereza kwani, unapokuja katika nchi lazima uiheshimu nchi na watu wake,” alisema wakala huyo na kuongeza: “Yaya alipokwenda Man City walikuwa na ndoto za kucheza Ligi ya Mabingwa na mastaa wakubwa walikuwa hawataki kwenda City, lakini Yaya alikuja na wakati huo hawakuwa na timu kubwa. Baada ya kuwasili walianza kushinda mataji na kuipeleka timu Ligi ya Mabingwa.

“City ina wachezaji wakubwa, lakini Guardiola anataka akina Yaya na Hart waondoke. Kwangu nawaheshimu makocha kama Claudio Ranieri ambao wametwaa mataji bila ya kutumia pesa nyingi.”

Kauli hizi kali za Seluk zilikuja muda mchache baada ya Guardiola kumshambulia yeye kwa kauli alizotoa baada ya kumuacha Yaya nje ya kikosi chake.

“Lilikuwa suala gumu sana kwangu kumuacha Yaya nje ya kikosi cha Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa sababu najua ni mtu mzuri. Lakini baada ya wakala wake kuongea, kuanzia siku hiyo Yaya sitamuhesabu tena. Mpaka Bwana Seluk alipokuja kuongea na vyombo vya habari au rafiki zake katika vyombo vya habari sitamuhesabu. Nadhani anaweza kuwa na moyo wa kwenda katika vyombo vya habari na kuiomba msamaha Man City kwanza,” alisema Guardiola juzi mchana.

“Msamaha wa pili ni kwa wachezaji wenzake na baada ya hapo kocha. Ikitokea hivyo Yaya atarudi kundini na atakuwa na nafasi ya kucheza mechi zote tena.

“Nikiwa kama kocha sipendi kila wakala ambaye mchezaji wake hachezi aende katika vyombo vya habari na kuongea sana.

“Kwa hali ilivyo inategemea sasa, najua Seluk anampenda sana Toure, kama ananipenda mimi aonyeshe kwa kuomba msamaha kwa Manchester City kwa alichofanya.

“Siwezi kufikiria wakati nilipokuwa nacheza soka, wakala wangu aende katika vyombo vya habari na kuongea vibaya dhidi ya Johan Cruyff (kocha wake wa zamani akiwa mchezaji Barcelona) kuhusu jambo hili au lile. Labda ni zama mpya sasa, vipindi vinabadilika, lakini mimi ni mtu wa kizazi cha zamani.

“Mawakala wa zamani walikuwa wanawaachia wachezaji wafanye kazi zao na makocha wafanye kazi zao, lakini mawakala wa siku wanajiona wao ni kila kitu. Kama ana matatizo angempigia Txiki Begiristain au klabu ili wazungumze. Kama Yaya hataongea basi hataichezea Man City tena.”