Uganda kura hazikutosha Afcon, inauma

UGANDA kwa sasa hata iichape Mali mabao 100 katika mchezo wao wa mwisho, pointi zao hazitatosha kuwavusha kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Afcon 2017 baada ya kukumbana na vichapo kwenye mechi zake mbili za kwanza za Kundi D.

Uganda imekubali kichapo cha bao 1-0 katika kila mechi ilipocheza na Ghana na kisha Misri na hivyo, kuwafanya wasiwe na pointi hata moja, huku kundi hilo Ghana wakiongoza kwa kuwa na pointi sita, wakifuatiwa na Misri wenye pointi nne huku Mali wana pointi moja na vijana wa Milutin ‘Micho’ Sredojevic, ambao hizi ni fainali zao za kwanza tangu mwaka 1978 hawana pointi hata moja.

Kwa matokeo hayo, Misri hata ifungwe mechi yake ya mwisho itakapocheza na Ghana, kisha wao Uganda wawafunge Mali, pointi zao haziwezi kutosha kuwavusha kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa sababu watakuwa na pointi tatu, labda kama tu itokee bahati ya kupenya kwa besti luza.

Kwenye mechi yao dhidi ya Misri, Uganda walicheza soka maridadi sana, huku kiungo wao Tony Mawejje akionyesha kiwango bora kabisa na sambamba na Geoffrey Kizito na Khalid Aucho, wakati mabeki wao Hassan Wasswa na Murushid Juuko waliounda kombinesheni nzuri iliyowapata shida washambuliaji wa Misri iliyoongozwa na Mohamed Salah.

Uganda ilipata bao, lakini likakatiliwa kwa kuwa mfungaji alikuwa ‘offside’, kabla ya wao kufunga bao katika dakika za mwisho kabisa na hivyo kupoteza mchezo. Uganda itakipiga na Mali mjini Oyem, Jumatano.