Wenger amzuia Ozil kwenda Man United

Muktasari:

Ishu imekuwa siriazi na kocha Jose Mourinho anafikiria hata kumpiga bei Henrikh Mkhitaryan kwa sababu anafahamu wazi atapata huduma ya Ozil, mchezaji ambaye anamfahamu vyema kabisa baada ya kuwa naye kwa miaka mitano walipokuwa kwenye kikosi cha Real Madrid.

LONDON, ENGLAND. STORI inayobamba huko kwenye korido za Emirates ni kuhusu Mesut Ozil kwenda Manchester United, lakini kocha Arsene Wenger amekurupuka na kujaa juu akisema "Hao Manchester United hawajaleta ofa yoyote kumtaka Ozil."

Ishu imekuwa siriazi na kocha Jose Mourinho anafikiria hata kumpiga bei Henrikh Mkhitaryan kwa sababu anafahamu wazi atapata huduma ya Ozil, mchezaji ambaye anamfahamu vyema kabisa baada ya kuwa naye kwa miaka mitano walipokuwa kwenye kikosi cha Real Madrid.

Ozil alikuwa na mtihani wa kuamua kwenda Man United au Barcelona, lakini mwenyewe ameshapata majibu kwamba safari ya Old Trafford itapendeza zaidi. Ozil aligomea mshahara wa Pauni 235,000 kwa wiki, ambao Arsenal ilimpa ofa akitaka mkwanja unaokaribia Pauni 300,000 kwa wiki, pesa ambayo Man United wanaweza kuimudu zaidi.

Mkataba wa Ozil huko Arsenal utakwisha mwisho wa msimu, hivyo staa huyo atakuwa huru kusaini mkataba wa awali na timu nyingine kuanzia Januari. Lakini, ni timu za ng'ambo kwa timu kama Man United, kama inataka ipeleke pesa Januari, au isubiri hadi mwisho wa msimu kumchukua bure staa huyo wa Kijerumani.

Lakini, Wenger anasema hivi: "Hapana. Hatujafuatwa na Manchester United. Atabaki hapa hadi mwisho wa msimu. Wote watabaki. Ni ngumu kuwaeleza, lakini mimi nina mitazamo yangu tofauti kwa kila jambo."

Wachezaji wengine ambao mikataba yao itakwisha mwishoni mwa msimu ni Alexis Sanchez, Aaron Ramsey na Jack Wilshere, hivyo Wenger ana shughuli pevu katika kuwabakiza mastaa hao. Arsenal leo Jumamosi itakipiga na Newcastle United katika mfululizo wa Ligi Kuu England ikijaribu kusaka ushindi wake wa kwanza baada ya mechi nne.