Wema ni malkia wa ‘comeback’ kwa Diamond Platnumz

Muktasari:

Imeshathibitika kuwa inawezekana kabisa kumpokonya Wema tonge mdomoni. Ukitaka kumjua Wema ni nani kwa Diamond, waulize Jokate Mwegelo, Penniel Mungilwa ‘Penny’ na sasa mrembo cheupe wa Uganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, amesalimu amri.

Kuna watu hawajawahi kushindwa. Miss Tanzania 2006 na staa mkubwa wa filamu Bongo, Wema Sepetu hana rekodi ya kushindwa. Ndiyo, Wema hajawahi kupoteza pambano kwenye vita ya kuwania penzi la kiongozi wa WCB, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Imeshathibitika kuwa inawezekana kabisa kumpokonya Wema tonge mdomoni. Ukitaka kumjua Wema ni nani kwa Diamond, waulize Jokate Mwegelo, Penniel Mungilwa ‘Penny’ na sasa mrembo cheupe wa Uganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, amesalimu amri.

Katika mahojiano ambayo Zari alifanya hivi karibuni na idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), ametamka mwenyewe kwamba pamoja na mengineyo, sababu ya mwisho iliyomfanya achukue uamuzi wa kuachana na Diamond ni picha ambazo zilivuja mitandaoni, zikimwonesha Diamond amekumbatiana na Wema.

Kwamba, kumbe Zari hajaamua kung’oka kwa Diamond kwa sababu ya baba watoto wake huyo kuzaa na mwanamitindo wa Bongo, Hamisa Mobeto. Aliyemkimbiza ni Wema. Ooh, kumbe Zari aliona bora Diamond kuzaa na Hamisa, maana alisamehe. Diamond kukumbatiana na Wema ameshindwa kuvumilia. Amemwaga manyanga.

Baada ya vishindo vyote na maonyesho ya kila aina, ilishaonekana Zari amemuweza Wema. Ikajengwa imani kwamba kiboko ya Wema ni Zari. Maana mfupa uliowashinda Penny na Jokate, ni kama Zari alionekana kuutafuna kiulani na kufikiriwa kwamba alielekea kuumeza. Kumbe haikuwa hivyo, Wema yuleyule amerudi. Amerejea sana!

Ni Wema yuleyule aliyeambiwa na Zari kwamba anaishi maisha bandia, kwamba mapenzi yake, magari na nyumba ni feki. Akasisitiza kuwa Wema amejaa ufeki.Ni huyohuyo aliyemuona na kumwita feki, ndiye amemkimbiza kwa baba wa watoto wake wawili.

Unaweza kushangaa, Wema tena! Hasa baada ya Zari na Diamond kuonekana kufika mbali mno katika mapenzi yao na ujenzi wa familia. Hata hivyo, ukitulia utakiri kwamba huyo ndiye Wema. Yeye hufanya kama Lennox Lewis alipokubali kichapo cha Hasim Rahman, KO ya raundi ya tano, Aprili 22, 2001, ndani ya Carnival City Casino, mjini Brakpan, Afrika Kusini.

Kwa kichapo hicho, Lewis alipoteza ubingwa wa dunia, uzito wa juu, mikanda ya WBC, IBF, IBO na Lineal kwa mkupuo. Hata hivyo, Rahman alidumu na ubingwa wake kwa miezi mitano kasoro siku tano, kwani Novemba 17, 2001, ndani ya Mandalay Bay, Paradise, Nevada, Marekani, raundi ya nne, mikanda yote hiyo ilirejea kwa Lewis.

Wema ni kama mfalme wa Boxing, Muhammad Ali. Alipoteza ubingwa wa dunia uzito wa juu alipokataa kwenda Vietnam kuitumikia Marekani katika Vita ya Vietnam miaka ya 1960. Alifungiwa kucheza Boxing kwa sababu ya msimamo wake kwamba asingeitumikia nchi ambayo ilikuwa inabagua na kuwakandamiza watu weusi.

Ali alipofunguliwa kucheza Boxing baada ya kushinda kesi mahakamani, alipotaka kurejesha taji lake la ubingwa wa dunia, alipokea kichapo kwa pointi, kutoka kwa Joe Frazier, pambano la raundi 15, lililofanyika Machi 8, 1971, Madison Square Garden (MSG), New York Marekani.

Huo ni mfano mdogo tu jinsi ambavyo mabingwa hupoteza mataji, lakini sifa yao kubwa ni kule kurejea kwao kwa kishindo, kwamba akirudi kutetea ubingwa au nafasi yake utapisha tu. Haimaanishi kwamba Wema amesharejea kwa Diamond, ila kung’oka kwa Zari, huku sababu akiwa yeye, hilo ni bonge la comeback.

Ni malkia wa comeback

Mwaka 2012, Wema alipigwa kikumbo na Jokate kwenye penzi la Diamond. Wema alihaha. Alimtisha Jokate. Alifanya mahojiano na vyombo vya habari kueleza na kulaani jinsi Jokate alivyoingilia uhusiano wake na Diamond. Wakati huo Diamond akaonekana kweli amedata kwa Jokate, hakujali wala kuonesha kumhurumia Wema na machozi yake.

Vile ambavyo Jokate maisha yake yasivyo na skendo, basi alishambuliwa kweli. Aliitwa mlokole feki. Kwamba alikuwa akijifanya muimba kwaya kanisani lakini anavizia mabwana wa watu. Jokate naye maskini, akawa anajitahidi kukanusha kwamba hakuwa kwenye mapenzi na Diamond.

Unacheza na Diamond? Wakati Jokate akijitahidi kukanusha, Diamond akaona mapenzi ya siri ya nini? Akaweka wazi kuwa Jokate ndiye mpenzi wake na Wema alikuwa kando. Wema kweli akakubali kishindo cha Jakate ambaye akawa mtawala wa muda wa moyo wa Diamond.

Machi 31, 2012, ikafanyika shoo kubwa ya Diamond, lilikuwa onesho la watu maalum. Kiingilio Sh50,000 kwa kichwa. Kiwango kikubwa mno wakati huo. Tamasha liliitwa Diamonds Are Forever. Watu waliitikia na Jiji la Dar lilipambwa na shamrashamra.

Usiku ndani ya Mlimani City, Dar, Diamond akiwa jukwaani anawajibika, watu wengi wakajitokeza kumtuza. Wema naye alipokolea muziki, akajisogeza jukwaani kumtuza. Heee! Diamond akagoma kupokea tuzo ya fedha kutoka kwa Wema. Basi Wema aliganda kubembeleza noti zake zipokelewe bila mafanikio.

Siku iliyofuata habari kubwa ikawa Diamond kumdhalilisha Wema kwa kukataa kupokea fedha alizojaribu kumtuza. Diamond akatokeza na kueleza kuwa Wema alitaka yeye apokee fedha ili apate ‘kiki’, kwamba ana fedha nyingi mpaka amempa yeye na kupokea. Wema alisema hakuwa na nia, bali alimpongeza kama shabiki.

Baadaye ikavuma kwamba Wema ndiye aliyemwandalia Diamond mavazi mpaka chakula kwa ajili ya shoo hiyo, kwa hiyo walikuwa kwenye wakati mzuri, isipokuwa tu Diamond aliamua kumgeuka mbele ya kadamnasi, kitu ambacho Wema hakuwa amekitarajia.

Ikabainika kwamba Diamond aliamua kukataa fedha za Wema ili kumwonyesha Jokate kuwa hawaivi. Ooh! Ule uumbuaji wa Diamond kwa Wema ulifanyika kwa hisani ya Jokate. Kwamba Jokate ajionee mwenyewe jinsi ‘boyfriend’ wake anavyomuumbua ‘X’ wake.

Unajua nini kilitokea? Wema alirejea kwa Diamond na Jokate alipisha njia. Wema aliporejea alitangaza utawala wake mpya na kila mtu alijua kwamba ‘mwenye mume’ alikuwa amerejea kwenye umiliki wake. Ni kweli Jokate alimpindua Wema kwa Diamond, lakini Wema alifanya bonge la comeback na kumng’oa Jokate.

Muulize Penny

Desemba 30, 2012, Diamond aliweka video kwenye chaneli yake ya YouTube, iliyomuonesha akicheza muziki na Penny, baada au kabla ya kuanza mahojiano kwenye kipindi cha X-Live, televisheni ya DTV. Mwenyeji wa kipindi hicho alikuwa ni Penny.

Uchezaji wao uliambatana na mabusu na kukumbatiana kiasi. Si Penny aliyembusu Diamond, isipokuwa Diamond ndiye alifanya hivyo. Mtoto wa kike naye akawa amejilegeza lakini mwenye kujiamini, kuonyesha kwamba aliyoyafanya Diamond hayakuwa mageni wala kulazimishwa. Aliridhia! Januari 2013 uvumi ukaanza kuwa Penny ndiye aliyeingia kwenye nafasi ya Wema. Februari 2013, Diamond alimtangaza Penny kuwa mrithi wa kiti cha Wema. Zikafuata zama za Diamond na Penny kung’ara na mapenzi yao. Kuna wakati waliudanganya umma kwamba wangefunga ndoa.

Siku moja usiku Wema alimpigia simu Diamond kuomba wayaweke sawa mambo yao. Ni kipindi ambacho Wema alikuwa akitambua fika kwamba Diamond alikuwepo kwenye mapenzi na Penny. Basi Diamond akapokea simu, akajiongelesha kidogo, halafu akampa Penny amalizane na Wema.

Wanawake wakazungumza. Wema angesema nini wakati aliumbuliwa? Alimpigia simu Diamond wake bila kujua yupo na Penny. Anaongea na Diamond, mara anasikia sauti ya kike. Ikabidi Penny atambe tu kwenye mazungumzo. Kwa kifupi Penny alimtaka Wema asiwasumbue. Penny akasema: “Tuache tulale Wema.”

Kumbe mazungumzo hayo Diamond aliyarekodi. Akayasambaza. Wema alipohojiwa na vyombo vya habari hakujitetea, aliishia tu kusema tatizo la Diamond ni ushamba na ana mambo ya Kiswahili. Hata kipindi kile alipoumbuliwa kupokea fedha jukwaani alipotaka kumtuza, Wema alisema Diamond ni mshamba na ana mambo ya Kiswahili.

Hivyo, Wema faraja yake kila alipokutana na pigo la Diamond ni kumwita mshamba na mwenye mambo ya Kiswahili. Diamond akaingia studio mwaka 2013, akafyatua wimbo Number One, uliotoka Septemba 2013. Mwishoni mwa wimbo huo, Diamond anatoa kibwagizo cha kumalizia wimbo (outro): “Na mtuache tulale.” Akirejea yale maneno ya Penny kwa Wema.

Januari 2014, Diamond alitoa wimbo Number One Remix akimshirikisha staa wa Nigeria, David Adeleke ‘Davido’. Mwisho wa wimbo huo, Diamond anaweka kibwagizo “acha movie iendelee”, naam, ni movie (sinema) yake na Wema ilikuwa ikiendelea. Kipindi hicho tayari Penny alikuwa ameshawekwa kando na Wema kushika usukani.

Huyo ndiye Wema, amemtingisha Mama T (Zari) mpaka ameachia mchuma. Kwa picha tu ya kukumbatiana. Huyo ndiye Wema aliyekubali vishindo vya Jokate na Penny, lakini aliporudi alimfurusha kila mmoja kwa wakati wake. Hivi sasa Zari kaondoka, swali ni je, atakaa yeye au atamwacha mwingine?

Wema hajawahi kushindwa vita ya kumgombea Diamond. Waulize Penny, Jokate na Zari. Hata hivyo, ni vizuri sana Diamond na Zari wakatulia walee watoto.