Waziri Mwakyembe aunda jopo la wasanii

Muktasari:

Pamoja na wadau wengine, Mwakyembe alimtaja Wakili Albert Msando kuwa mmoja kati ya wanakamati watakaounda jopo hilo, kwani amekuwa msaada mkubwa kwa kuwasimamia wasanii kisheria.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema anaunda jopo la wadau wa sanaa watakaojadili na kutoa mapendekezo katika mabadiliko ya sheria mpya ya sanaa ya muziki wa kizazi kipya nchini.

Pamoja na wadau wengine, Mwakyembe alimtaja Wakili Albert Msando kuwa mmoja kati ya wanakamati watakaounda jopo hilo, kwani amekuwa msaada mkubwa kwa kuwasimamia wasanii kisheria.

Akizungumza katika kikao cha mpango kazi ambacho lengo kuu ni kutoa fursa kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya  kujadili kwa pamoja ili kukuza sanaa nchini.

"Nitaunda jopo la kujadili mapendekezo ya sheria mpya na nitahakikisha nitasimamia mwenyewe muswada huo ili upitishwe katika bunge linaloshindikana," alisema Mwakyembe.

Aidha alitoa onyo kwa mameneja wanaonyonya wasanii wa muziki kwa kuwapa mikataba mibovu isiyoeleweka watakiona cha moto kupitia sheria na Sera ambayo inaandaaliwa kwa ajili ya kutetea haki za wasanii.

Katibu wa Chama cha Wasanii wa muziki wa kizazi kipya (TUMA), Samwel Mbwana alisema hawaridhishwi na utendaji kazi wa Chama cha Hakimiliki Tanzania(Cosota) kwa kuwa wameshindwa kusimamia haki zao na kuomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwachunguza.

Alisema Cosota imekuwa ikipata fedha kupitia wao, lakini wao hawanufaiki na kazi zao hali ambayo imewanyima kushindwa kufaidi haki zao na kumuomba waziri Mwakyembe kuwasaidia.

Pia, aliomba kuwepo na sera za kulinda muziki wao ili upewe nafasi ya kupigwa katika maeneo husika pasipo kuwa na upendeleo.

Afisa Kodi Mkuu TRA, Sudney Mkamba alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kipindi cha miaka miwili tangu urasimishaji wa kazi za sanaa, wamekamata CD feki zilizokuwa na stempu za kughushi takribani milioni moja.

"Kwa kushirikiana na wasanii na Cosota tuliamua kufanya msako dhidi ya wanaodurufu stempu za kughushi na kubandika katika CD feki tulifanikiwa kukamata CD milioni moja ambazo kupitia hizi serikali ilikuwa ikikosa Mapato," alisema Mkamba.

Hata hivyo, Mkamba alitoa wito kwa wasanii nchini kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa hasa zihusuzo usajili.

Kikao hicho cha mpango kazi kiliwashirikisha wasanii, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Chama cha Hakimiliki (Cosota), Wakala wa usajili (Brela) na British Council.