Wawili Prisons wapelekwa Yanga

Muktasari:

  • Bares kwanza amesisitiza kuwa hataki mchezaji wake hata mmoja aondoke kwenye timu hiyo, lakini amekuwa mkweli na kuwaelezea wachezaji hao ambao ni Eliuter Mpepo, Mohamed Rashid, Salum Kimenya na mlinda mlango Aron Kalambo kuwa wanastahili kupata timu kubwa zaidi.

MSIMU wa Ligi Kuu Bara uko ukingoni ambapo timu na wachezaji huwa wanaangalia sehemu ya kupata malisho mazuri kwa msimu ujao, na sasa Kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohamed ‘Bares’ amewapa nyota wake wanne mchongo wa maana.

Bares kwanza amesisitiza kuwa hataki mchezaji wake hata mmoja aondoke kwenye timu hiyo, lakini amekuwa mkweli na kuwaelezea wachezaji hao ambao ni Eliuter Mpepo, Mohamed Rashid, Salum Kimenya na mlinda mlango Aron Kalambo kuwa wanastahili kupata timu kubwa zaidi.

Kocha huyo Mzanzibari alifichua kuwa anajua timu mbalimbali zimeshaanza kuwanyemelea wachezaji hao kama Simba, Yanga na Azam na kusema Mpepo na Mohamed wasifanye haraka ya kuondoka kikosi hapo ili wapate uzoefu zaidi na kama watashindwa kabisa kuvumilia, timu ambazo wanaweza wakapata nafasi ya kucheza kutokana na stahili yao ya uchezaji ni Azam na Yanga lakini si Simba.

Akawataja Kimenya na Kalambo na kusema, kutokana na uzoefu wao wa kutosha na wana uwezo wa kucheza timu yoyote kwenye ligi kuu na wakafanya vizuri.

“Kiuhalisia kama kocha, sipendi mchezaji hata mmoja aondoke Prisons, wale waliopo sasa niendelee nao kwa msimu mwingine.”