Watakaokatwa katika uchaguzi wa TFF kujulikana mapema tu

Muktasari:

Majina ya waliopitishwa na wale waliorudishwa kujipanga upya huenda yakatangazwa keshokutwa Jumamosi.

Dar es Salaam. Kikao cha kuwapitisha na kuwakata wagombe wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kinamalizika kesho Ijumaa.

Majina ya waliopitishwa na wale waliorudishwa kujipanga upya huenda yakatangazwa keshokutwa Jumamosi.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF imejifungia kwa siku tatu katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam ikiwa na wajumbe watano na inaongozwa na Mwanasheria, Revocatus Kuuli.

Kuuli alisema hakuna changamoto kubwa waliyokumbana nayo kwenye kupitia fomu 74 za wagombea wa Urais, Makamu wa Rais na wajumbe wa uchaguzi huo zaidi ya kuhitaji umakini mkubwa kupitia ili kila mgombea ajiridhishe na kile kitakachoamuliwa na kamati hiyo.

"Changamoto iliyopo sio kubwa sana zaidi ya fomu kuwa nyingi, ila mengine ni ya kawaida, tulipanga kutangaza majina keshokutwa (kesho) lakini hatuna uhakika sana kama tutangaza siku hiyo ila uhakika ni Jumapili. Tumepanga Jumamosi kupitia tena ili tujiridhishe na kile tulichokifanya ili kusiwemo na malalamiko.

"Unajuwa ili watu wakuamini ni lazima ufanyekazi kwa uangalifu mkubwa, ujiridhishe ndipo utoe uamuzi wa kile ulichokifanya, sisi tunajiamini na kila kitu kitakuwa sawa kabisa, katika maamuzi yetu hatuingiliwi na mtu yoyote kila mgombea atapata haki yake," alisema Kuuli.