Walangua tiketi wakiona cha moto

Muktasari:

Tofauti na hapo awali ambapo kampuni hiyo iliweka watu wa kuuza kadi pamoja na tiketi za kuingilia uwanjani kwenye maeneo mbalimbali yanayozunguka uwanja huo, jana ilikuja na utaratibu wa mawakala wake kuuza kadi na tiketi wakiwa ndani ya uzio wa uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru jijini, huku ikitoa matangazo ya kuwataka watu kutonunua kadi hizo kutoka kwa watu walio nje ya uzio.

MCHEZO wa Simba na Yanga jana, pengine ulikuwa na mkosi kwa walanguzi wa tiketi waliokuwa na tabia ya kupandisha bei ya tiketi za kuingilia Uwanja wa Taifa kutazama mechi, baada ya kampuni ya Selcom kuweka utaratibu uliosaidia kudhibiti kwa kiasi kikubwa watu hao.

Tofauti na hapo awali ambapo kampuni hiyo iliweka watu wa kuuza kadi pamoja na tiketi za kuingilia uwanjani kwenye maeneo mbalimbali yanayozunguka uwanja huo, jana ilikuja na utaratibu wa mawakala wake kuuza kadi na tiketi wakiwa ndani ya uzio wa uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru jijini, huku ikitoa matangazo ya kuwataka watu kutonunua kadi hizo kutoka kwa watu walio nje ya uzio.

Mbinu hiyo ilionekana kuzaa matunda kwani kundi kubwa la mashabiki lilifuata utaratibu huo uliowekwa ingawa wachache walinunua tiketi na kadi hizo kwa bei ya juu tofauti na ile iliyopangwa, kutoka kwa walanguzi wachache ambao waliuza kadi na tiketi hizo kwa kujificha tofauti na ilivyozoeleka hapo awali.

"Tunamjali mteja na ndio maana tumekuwa tukitangaza na kuweka matangazo ya bei halisi ya kadi pamoja na tiketi iwe wazi na  wateja wetu wasilanguliwe kama ambavyo wamekuwa wakifanyiwa siku za nyuma. Tunaendelea kuwasisitiza mashabiki kununua tiketi kwa bei ileile iliyoelekezwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)," alisema mmoja wa mawakala wa kampuni hiyo.

Katika kuonyesha ni kwa namna gani Selcom, TFF pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama jana vilijipanga kuhakikisha suala hilo linakomeshwa, baadhi ya vijana ambao waliruka uzio na kuingia ndani ya uwanja na kujifanya ni mawakala wa kampuni hiyo ili wawanase kirahisi mashabiki, walitiwa nguvuni na maofisa wa jeshi la Polisi waiodumisha ulinzi ndani ya eneo hilo.