Wakitua tu, Man UTD haitashikika

Muktasari:

  • Kwanza ni upande chanya, kwamba imemaliza Ligi Kuu England ikiwa nafasi ya pili na kama watakuwa wamefanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la FA, basi hilo litawafanya kuwa wamefanikiwa zaidi kama ukilinganisha na msimu uliopita.

KWA msimu huu Manchester United unaweza kuitazama katika namna mbili kuu.

Kwanza ni upande chanya, kwamba imemaliza Ligi Kuu England ikiwa nafasi ya pili na kama watakuwa wamefanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la FA, basi hilo litawafanya kuwa wamefanikiwa zaidi kama ukilinganisha na msimu uliopita.

Pili ni upande hasi, ambapo imetumia pesa nyingi kufanya usajili lakini imeshindwa mbele ya mahasimu wake Manchester City, tena ikiachwa kwa pointi nyingi kwenye msimamo wa ligi huku ikitupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema tu, hatua ya 16 bora tu. Inahuzunisha.

Lakini, kwa matokeo yoyote yale, ukweli unabaki kuwa mmoja tu, Man United inapaswa kufanya vizuri wakati wote.

Na kwa sababu kocha Jose Mourinho haonekani kuwa na mpango wa kuiacha timu hiyo, basi kuna matumaini makubwa kwamba United itafanya uwekezaji mkubwa zaidi kwenye kikosi chake kwa kusajili kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Katika misimu miwili iliyopita, Man United, ilitumia karibu Pauni 150 milioni kwa kila msimu na kuna uwezekano mkubwa kiwango kama hicho cha pesa kikatumika tena kwenye dirisha hili ili kunasa wachezaji watakaokuja kuweka tofauti kwenye kikosi hicho cha Man United.

Hii hapa orodha ya wachezaji watano ambao hakuna mashaka kabisa kwamba wakinaswa tu na Man United basi wataweza kuchuana na Man City kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao.

Danny Rose

Beki wa kushoto, Danny Rose, amepambana na hali yake juu ya utimamu wake wa ndani ya uwanja, lakini bado ni mchezaji mahiri kweli kweli kwenye nafasi yake.

Beki ya kushoto ni shida kwenye kikosi cha Man United hasa baada ya Luke Shaw kushindwa kucheza kwa kiwango kinachopaswa jambo hilo linalomfanya kocha Mourinho awe anamtumia zaidi Ashley Young, ambaye ameonyesha kiwango bora na kupata nafasi ya kuwamo ndani ya kikosi cha England kitakachokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia litakaloanza mwezi ujao kule Russia.

Man United inahitaji huduma ya Danny Rose kwa sababu asipokuwa majeruhi, ni beki mmoja wa pembeni matata sasa.

Gareth Bale

Supastaa, Gareth Bale, ni jina linalotajwa muda mrefu sasa likihusishwa na Manchester United, lakini hilo ni jambo zuri. Licha ya kuwapo na wasiwasi juu ya ufiti wake, lakini staa huyo wa kimataifa wa Wales ni mchezaji mwenye ujuzi, kasi na nguvu ya kutosha kuibeba timu kwenye mechi kubwa na ngumu.

Hakuna ubishi, Man United, inahitaji mchezaji wa pembeni kwenye safu yake ya ushambuliaji ili kuongeza kasi kwenye eneo hilo na ndiyo maana kwenye dirisha lililopita ilihangaika kuinasa huduma ya Ivan Perisic wa Inter Milan.

Zile krosi za Bale zitakuwa msaada mkubwa kwa straika Romelu Lukaku na zitamfanya awe anafunga tu na kuisaidia timu.

Toby Alderweireld

Licha ya kwamba Man United imemaliza msimu wa Ligi Kuu England ikiwa timu ya pili iliyokuwa na beki imara ikiruhusu bao moja tu zaidi ya mabingwa Manchester City, hakuna ubishi bado inahitaji kusajili beki wa kati atakayeipa uhakika zaidi wa uimara katika nafasi hiyo. Kumekuwa na makosa ya kizembe ambayo yamekuwa yakifanywa na mabeki wa Man United kama vile Phil Jones na Chris Smalling, huku ufiti pia ukiwa shida kubwa.

Eric Bailly kwa upande wake msimu huu amekumbwa na majanga ya kuwa majeruhi, sawa na Marcos Rojo, huku Victor Lindelof bado hajazoea mikikimikiki na mfumo wa Man United.

Kwenye kundi hilo la mabeki, Man United inahitaji kumwongeza mtu kama Alderweireld ili kuifanya kuwa imara zaidi kwa sababu inasemwa hivi ‘washambuliaji wanafunga mabao, mabeki wanaleta ubingwa’.

Toni Kroos

Kiungo wa Kijerumani, Toni Kroos, alihusishwa sana na mpango wa kujiunga na Man United kabla hata hajaenda Real Madrid.

Mjerumani huyo tangu alipotua kwenye kikosi cha Los Blancos, ameshinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja la La Liga na ripoti zinadai kwamba Real Madrid ipo tayari kumfungulia mlango wa kutokea kwenye dirisha hili la usajili wa majira ya kiangazi.

Mchezaji mwenyewe pia amedaiwa kuwa na mpango wa kuachana na timu hiyo huku Ligi Kuu England ikitazamwa kuwa mwelekeo wa kiungo huyo.

Pasi zake matata kwenye ile sehemu ya kiungo ni kitu ambacho Man United inakihitaji na akitua hapo ataweza kutengeneza kombinesheni matata kabisa ya viungo watatu sambamba na Nemanja Matic na Paul Pogba.

Thiago Alcantara

Kama ilivyo kwa Toni Kroos, Thiago, naye alikaribia kabisa kujiunga na Man United.

Lakini, kama ilivyokuwa kwa staa wa Real Madrid, Thiago na yeye aliamua kutimkia Bayern Munich wakati huo alipoondoka Barcelona. Lakini, ukweli utaendelea kuwa vilevile kwamba Man United bado inahitaji huduma ya wachezaji hao na kama itafanikiwa kuwanasa, basi watakuwa wameondoa pengo kubwa la ubora baina yao na mahasimu wao Man City.

Thiago Alcantara ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, kitu pekee kinachomkwamisha ni kuwa na bahati mbaya ya kuwa majeruhi mara kwa mara kwa siku za karibuni.

Akiungana na Pogba, hakika kombinesheni yao itasababisha matatizo makubwa kwa timu pinzani ndani ya uwanja.