VIDEO: Wafanyakazi MCL wanogesha Dasani Marathon

MWENYEKITI wa Chama cha Mpira wa Soka Dodoma, Mlamu Ng’ambi amekuwa miongoni mwa wanariadha waliojitokeza katika mbio za Dasani Marathon zilizofanyika jijini Dar es Salaam leo Jumapili, huku wafanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wakifukuza upepo katika mbio za kilometa kumi na 21.

Miongoni mwa wafanyakazi wa MCL, Msimamizi wa Usafirishaji, Philip Lingo aliyekimbia Kilomita 21 na kujinyakulia medali pamoja  na Afisa Masoko Kanda ya Dar es Salaam,  Jackson Ngassa aliyekimbia kilomita 10.

Mbio hizo zinazodhaminiwa na makampuni mbalimbali ikiwemo Dasani, Mwananchi Communications Limited (MCL), NMB, ziliwajumuisha wanariadha mbalimbali  kutoka Tanzania na Kenya pamoja na watu binafsi kutoka ndani ya makampuni yaliyodhamini mashindano hayo.

Akizungumzia kushiriki katika Mashindano hayo, Ng’ambi alisema kwamba anajisikia furaha kushiriki mashindano hayo na amekuwa akishiriki mara kwa mara ili kuufanya mwili wake uwe na nguvu wakati wote.

“Leo nimekimbia kilomita ishirini na moja na hii ni mara yangu tangu yaanze mashindano haya, ikitokea sijashiriki basi huwa naumwa lakini mimi ni miongoni mwa wafanya mazoezi na nakimbia sana kutokana tuna chama chetu,” alisema.

Wakati huo huo Mratibu wa Mashindano hayo, Goodluck Davies, alisema kwamba mwaka huu wamejitokeza watu wengi ikiwemo makundi mbalimbali tofauti na miaka ya nyuma kuwa na watu binafsi wengi.

“Mwaka huu umekuwa mwaka wa tofauti sana kwa sababu watu wamejitokeza wengi, sio mwisho wa mashindano haya lakini tutakuwa na mbio za nyika zitafanyika kipindi cha Christmas Desemba,” alisema.

Washindi wa Kilomita 21 kwa upande wa Wanawake, wa kwanza Esther Chesang (Kenya) (2:15:18), Failuna Abdi (Arusha) (2:15:42), Jackline Sakilu (Arusha) (2:19:22), Monika Cheruto (Kenya) (2:32:43), Samantha Leader (DSM), 2:42:92, Molly Freeman (Dsm) (2:57:18), Jamila Abdula (Dsm) (3:02:12), Anjela Mandi (Dsm) (3:06:17), Ma Pilau (Dsm) (3:08:04) na Lucia Minde (Dsm) (3:11:18).

Kwa Upande wa Wanaume Bernard Musau (Kenya) (1:03;15), Evans Kurui (Kenya) (1:03:19), Festas Cheboi (Kenya) (1:03:21), Paul Muithya (Kenya), (1:03:22), Ezekiel Ngimba (Arusha) (1:03:29), Marko Joseph (Singida) (1:03:32), Agustino Sulle (Arusha) (1:04:07), Josephat Kiploech (Kenya) (1:04:17), Nestory Steven (Singida) (1:04:44) na Pascal Mombe (Arusha) ambaye alikimbia kwa saa 1:05:04.

Kwa upande wa walemavu ambao walikimbia kilomita 21, nafasi ya kwanza ilishikwa na Shukuru Khalfan, David Mabula alishika nafasi ya pili huku nafasi ya tatu ikishikwa na John Stephen (wote Dar es Salaam).

Washindi wote katika Mashindano haya walijinyakulia viwango tofauti vya fedha taslimu ambazo zilikuwa kama zawadi kwao ili kuwatia morali.