Wachezaji Alliance Girls wachezea kipigo usiku

Muktasari:

Taarifa zilizotolewa na mmoja wa  wachezaji hao, ambaye hawakutaka jina lake litangazwe amesema usiku wa kuamkia Alhamisi walikumbana na kipigo cha aina yake baada ya kuomba kupewa likizo kama walivyoahidiwa na uongozi wa kituo hicho.

Mwanza. Katika hali isiyo ya kawaida wachezaji wa klabu ya Alliance Girls usiku wa kuamkia jana Alhamisi walijikuta katika wakati ngumu kwa kutembezewa bakora na uongozi kwa madai ya kuomba ruhusa ya kwenda likizo.

Taarifa zilizotolewa na mmoja wa  wachezaji hao, ambaye hawakutaka jina lake litangazwe amesema usiku wa kuamkia Alhamisi walikumbana na kipigo cha aina yake baada ya kuomba kupewa likizo kama walivyoahidiwa na uongozi wa kituo hicho.

Amesema awali waliahidiwa kupewa zawadi iwapo watashinda mchezo wao dhidi ya Sisterz FC ambao walishinda, lakini walipohoji na kuomba kupewa likizo baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Wanawake wakakumbana na kipondo kikali.

"Tulipigwa mno na sasa tumelala na hamu ya kula hatuna, kikubwa tulienda kuomba kupewa likizo na zawadi tuliyoahidiwa kama tutashinda mechi yetu na Sisterz, lakini tulichoambulia ni kipigo kutoka kwa viongozi" amesema mchezaji huyo.

Amesisitiza kuwa hadi sasa ni mwaka wa tatu hawajaenda likizo na kwamba wao wanachohitaji ni kwenda makwao kusalimia hata wazazi wao.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Mashindano ya Klabu hiyo,Yusuph Budodi amesema kuwa yeye hajui hilo tukio na kwamba anachojua ni baada ya kumalizika kwa Ligi, walivunja kambi na wachezaji ambao ni wanafunzi shuleni hapo wakaendelea na mitihani.

"Hilo tukio silijui labda kama ni mambo ya utawala tofauti na idara yangu, nachoweza kusema ni kwamba tulipomaliza Ligi tulivunja kambi wanafunzi wakaendelea na mitihani" amesema Budodi.

Hata hivyo Mkurugenzi wa kituo hicho, James Bwire alipotafutwa amesema yeye hajui lolote licha ya kupigiwa simu kumuuliza suala hilo na kusema kuwa atafutwe baadaye.

"Mimi hilo suala hilo silijui, napokea simu tofauti naulizwa, lakini sijui kabisa lakufanya nitafute tena baadaye nitakuwa nimetulia," amesema Bwire.