WC2018: Usain Bolt aitabiria Argentina ubingwa

Wednesday June 13 2018

Mwamba wa mbio za mita 100, Mjamaica Usain

Mwamba wa mbio za mita 100, Mjamaica Usain Bolt, ameitabiria ubingwa timu ya Argentina katika mashindano ya Kombe la Dunia. 

By Fadhili Athumani

Moscow, Russia. Mwamba wa mbio za mita 100, Mjamaica Usain Bolt, ameitabiria ubingwa timu ya Argentina katika mashindano ya Kombe la Dunia, yatakayoanza kesho nchini Russia.

Bolt, ambaye hivi karibuni ilidaiwa kuwa anahamishia majeshi yake katika ulimwengu wa soka, pia ni muumini mkubwa wa Lionel Messi na kwa mujibu wa kaulo yake mwenyewe, amesema huu ni mwaka wa Messi kuionesha dunia yeye ni nani.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, bingwa huyo mara nane wa Olimpiki, alisisitiza kuwa yeye ni shabiki wa Lionel Messi kutoka kitambo na kwa maana hiyo, anaenda Russia akiwa nyuma ya Argentina na kuongeza kuwa huu ni mwaka wa Lionel Messi.

"Binafsi naishabikia Argentina, nimekuwa shabiki wa Messi kutoka kitambo, naamini tunaenda Russia kubeba kombe, kwa kikosi hiki, tuna nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa, itakuwa ni burudani tu," alisema Usain Bolt.

Argentina, ambayo imepania kutwaa ubingwa kwa nyingine tangu ifanye hivyo mwaka 1986,  imepangwa katika kundi D pamoja na Iceland, Croatia na Nigeria.

Aidha, Argentina inatajwa miongoni mwa mataifa yanayopigiwa upatu kuivua ubingwa, bingwa mtetezi Ujerumani hasa ikizingatia ubora wa kikosi chao na uwepo wa Lionel Messi uwanjani, licha ya kupata tabu katika kampeni ya kusaka tiketi ya kwenda Russia.

Mbali na Argentina mataifa mengine yanayopewa nafasi kutesa nchini Russia ni pamoja na Brazil, Spain, Germany na  France huku kutoka Afrika kila mtu anaitizama Misri ya Mohammed Salah na Essam El-Hadary.