Takukuru yamkamata mgombea TFF

Saturday August 12 2017

 

By Thobias Sebastian na Matereja Jalilu

Dodoma. TAASISI ya Kupambana na kuzuia Rushwa (TAKUKURU) inamshikilia mgombea ujumbe nafasi ya uwakilishi kanda namba nane, Yono Stanley.

Mgombea huyo anayewania nafasi ya kuwakilisha mikoa ya Ruvuma na Njombe ameshikiliwa na kuhojiwa na taasisi hiyo akidaiwa kutaka kutoa rushwa kwa wajumbe ili wamchague kinyume na sheria.

Taarifa za kushikiliwa pamoja na kuhojiwa kwake zimethibitishwa na Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, RPC Ramadhan Mambosasa ambapo amesema mgombea huyo amekutwa na Sh.500,000.

Mambosasa ameongeza kuwa mgombea huyo amekutwa msalani ndani (chooni) nje ya ukumbi wa uchaguzi na alikuwa amezigawa kwenye bahasha zenye kiasi cha Sh 50,000 kwa kila bahasha.

"Ni kweli mgombea huyo anashikiliwa na kuhojiwa na Takukuru kwa tuhuma za kutaka kutoa rushwa kwa wapiga kura ambazo alikutwa na pesa msalani (Chooni), akikutwa na hatia ya kufanya jambo hilo la nia ya kutoa  rushwa sheria zitachukuliwa," alisama Mambosasa.