Stand United wakija Taifa lazima mtacheka sana

Muktasari:

“Jambo la kwanza, tumehakikisha wanayazoea mazingira ya mjini hapa Shinyanga kabla ya kusafiri kwenda mikoa mingine,” alisema Bilo.

BAADA ya Stand United ‘Chama la Wana’  kusajili wachezaji nyota kutoka vijijini  walikokuwa wanafanya kazi ya kilimo, wameamua kuwaandalia programu maalumu itakayofanya  kuendana na uhalisia wa Ligi Kuu Bara.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Athuman Bilali ‘Bilo’ ndiye alifanya usajili huo, kabla ya ujio wa kocha mkuu, Mrundi Niyongabo Amars, ambaye alikuwa anafundisha timu ya Bujumbura City. Sikia atakachofanya Bilo kwa wachezaji hao.

“Jambo la kwanza, tumehakikisha wanayazoea mazingira ya mjini hapa Shinyanga kabla ya kusafiri kwenda mikoa mingine,” alisema Bilo.

“Hilo limefanikiwa, kwani kwa sasa wamekuwa wajanja, labda tukicheza mechi ya ligi pale Uwanja wa Taifa ndio watashangaa uwanja wa Dar es Salaam, kwa sekunde kadhaa, kitakachofuata iwe tumecheza na Simba ama Yanga, ni kuwashangaza mashabiki wao.

“Hawa jamaa wanaujua mpira, timu kubwa zitashangaa zenyewe.

“Tuliwasajili kutoka vijijini, kwanza walikuwa wanaitamani Stand United na sasa wameipata nafasi hiyo, hivyo kila mmoja wao amepania kuhakikisha anajenga jina. Kwa sasa tunasubiri tucheze na Kahama Kombaini kabla ya kuiwahi Mtibwa Sugar.”