Simba kuanza Bocco, Okwi, Kagere kwa Ndanda

Muktasari:

Mabingwa hao watetezi wameshinda mechi zao mbili za mwanzo wa Ligi Kuu

Mtwara. Kocha wa Simba, Patrick Aussems amepania kushinda kwa mabao mengi kesho kutokana na lengo lake kuanzisha kwa pamoja  washambuliaji wake watatu John Bocco, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Mbinu ya kocha huyo kuendeleza rekodi ya ushindi dhidi ya Ndanda ilionekana katika mazoezi waliyokuwa wakifanya jioni hii kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Katika mazoezi hayo kocha Aussems amewagawa katika timu mbili tofauti na huenda kikosi kimoja ndio kikaanza kesho.

Timu ya kwanza ina wachezaji Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mohammed Ibrahim, John Bocco, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Kikosi hiki ndio kinaweza kuwa kikosi cha kwanza kuelekea katika mechi ya kesho Jumamosi dhidi ya Ndanda.

Kikosi kingine kina Deogratious Munishi 'Dida', Adam Salamba Cleatus Chama, Said Ndemla, James Kotei, Poul Bukaba, Nicholas Gyan Rashid Juma na Marcel Kaheza.

Kikosi hiki kinaweza kuwa wale wachezaji wa akiba ambao watakuwa katika benchi dhidi ya Ndanda kesho.

Simba wanaingia katika mechi na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona huku wakiwa hawana rekodi ya kupoteza katika uwanja huo wala kufungwa na Ndanda tangu walivyopanda Ligi 2015.