Silaha mpya za Zahera Jangwani

Mwinyi Zahera

Muktasari:

  • Akizungumza jana Ijumaa katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Zahera alisema kutokana na mampumziko ya wachezaji wake, amezuia ujio wa wachezaji hao 10, lakini kati ya hao kuna wanne anaowajua vyema ambao hana shaka watakuja kumalizana na klabu hiyo endapo watakubaliana.

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera, amethibitisha uwezekano wa kikosi chake kushiriki Kombe la Kagame ni mdogo akisema ni kutokana na ratiba kuingiliana na programu ya mapumziko ya wachezaji wake, lakini akasema kuhusu usajili ana wachezaji 10 watakaojaribiwa na wanne tu ndiyo wenye uhakika wa moja kwa moja kusaini mikataba.

Akizungumza jana Ijumaa katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Zahera alisema kutokana na mampumziko ya wachezaji wake, amezuia ujio wa wachezaji hao 10, lakini kati ya hao kuna wanne anaowajua vyema ambao hana shaka watakuja kumalizana na klabu hiyo endapo watakubaliana.

Zahera alisema katika wachezaji hao wanne wawili ni mastraika hatari kushinda straika yeyote aliyepo sasa katika kikosi chake na kwamba anataka kuhakikisha safu ya ushambuliaji yake inaundwa na wachezaji bora wenye uwezo sawa.

Kocha huyo ambaye jana alitarajiwa kurudi kwake Ufaransa kwa mapumziko mafupi, alisema mbali ya mastraika hao pia katika idadi hiyo ya hao wachezaji wanne, mmoja ni winga anayejua kulisha washambuliaji akificha kabisa kutaja ni wa upande upi.

Alisema mwingine aliyesalia ni kiungo wa kati mchezeshaji anayekuja kusaidiana na Papy Kabamba Tshishimbi kutengeneza safu imara ya kiungo ambao wote watashuka nchini mara baada ya kumalizika kwa mapumziko.

“Nina orodha ndefu ya wachezaji wanaokuja hapa, wanafika 10 hao nilitaka waje ili tuangalie viwango vyao na baadaye tuamue. Katika hao, wanne tu ndiyo ninaowafahamu na hao hawatakuja kujaribiwa, kama watakubaliana na uongozi watasaini moja kwa moja,”alisema Zahera.

“Niliona hakuna sababu ya kuwaleta sasa kwa vile timu ipo mapumzikoni, kama tukiwaleta sasa inakuwa kama tunaingiza hasara kwa klabu kwa kuwagharimia malazi.

“Kati ya hao wawili ni washambuliaji wenye uwezo mkubwa na mmoja ni winga, sikwambii wa upande gani na mmoja aliyebaki ni kiungo wa kati anayekuja kushindana na kina Papy.”

Wanaoingia CAF

Aidha Zahera alisema anatambua katika mashindano ya Afrika wanatakiwa kuongeza wachezaji watatu tu ambapo hesabu zake ni kwamba watafanya usajili wa kutulia wakiangalia mbali nje ya mashindano ya kimataifa pia.

“Kumbuka msimu ujao tutakuwa na ligi pia kuna tutakaowaingiza CAF na wengine tutawasajili kwa ligi ya ndani maisha yaendelee.”

Kagame Yanga haimo

Akizungumzia ushiriki wa Yanga katika Kagame, Zahera alisema: “Yanga kikosi chetu si kipana, kuna wachezaji muhimu hawapo, itatulazimu kujumuisha vijana kushindana na wazoefu,” alisema Zahera.

“Tuliruhusu timu kucheza SportPesa pekee, hatuwezi kupeleka timu Kagame.”