Rekodi ya Kagere tishio kwa Ndanda

Muktasari:

Kagere amesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya

Mtwara. Mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere ameanza kuinyima usingizi Ndanda katika mechi ya kesho Jumamosi kutokana na rekodi yake  ya kuzifumania nyavu.

Kabla ya kucheza mechi ya kesho na Ndanda, Kagere tayari ameshafunga katika mechi tano mfululizo za kimashindano na kuwazidi nyota wengine wa Simba akiwemo, Emmanuel Okwi.

Kagere amefunga katika mechi ya fainali ya Kombe la Kagame Simba wakipoteza kwa mabao 2-1, dhidi ya Azam, alifunga bao lingine katika mechi ya Ngao ya hisani dhidi ya Mtibwa Uwanja wa CCM Kirumba, Simba walishinda 2-1.

Baada ya hapo Kagere alifunga tena katika mechi mbili za ligi dhidi, ushindi bao pekee dhidi ya Tanzania Prisons, mabao mawili dhidi ya Mbeya City waliposhinda 2-1.

Kagere alimaliza kasi hiyo katika mechi ya timu yake ya Taifa Rwanda dhidi ya Ivory Coast, bao lake pekee lilifanya matokeo ya 2-1.

Huenda Kagere ndio akawa nyota wa kuchungwa zaidi katika mechi ya kesho kuliko mchezaji yeyote yule wa Simba.

Simba wanaingia katika mechi na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona huku wakiwa hawana rekodi ya kupoteza katika uwanja huo wala kufungwa na Ndanda tangu walivyopanda Ligi 2015.