Omog, Simba ni mbingu na ardhi

Muktasari:

  • Omog anawaza kuitengeneza Simba itakayoweza kushindana katika mashindano ya kimataifa mwakani lakini watu wa Simba wanataka timu ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu. Inachekesha kidogo.

Dar es Salaam. KUNA jambo moja linaweza kuhitimisha maisha ya Kocha Joseph Omog ndani ya kikosi cha Simba. Ni tofauti ya fikra na malengo iliyopo kati ya Omog na watu wa Simba.

Omog anawaza kuitengeneza Simba itakayoweza kushindana katika mashindano ya kimataifa mwakani lakini watu wa Simba wanataka timu ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu. Inachekesha kidogo.

Omog anawaza kuwa na timu ya kushinda mechi kwa idadi yoyote tu ya magoli, watu wa Simba wanataka timu ya kushinda kwa kishindo, tena kila mechi. Kuna tofauti kubwa ya mawazo baina ya wawili hawa.

Omog anafahamu kuwa kwenye soka hata ukiwa na kikosi cha aina gani bado itafikia wakati utafungwa, lakini watu wa Simba wanaamini kuwa kwa timu waliyonayo kwa sasa hawatakiwi kufungwa kabisa. Kuna mkanganyiko mkubwa.

Omog anafahamu kuwa ukiwa na kikosi kipana unatakiwa kufanya mzunguko wa wachezaji ili kuwasaidia kulinda viwango vyao, lakini pia kuwa na watu wanaoweza kuziba nafasi pindi kunapotokea uhitaji lakini watu wa Simba wanataka wachezaji wao walewale wacheze kila siku.

Mwisho wa siku kunaonekana kuwa na tofauti kubwa kati ya Omog na watu wa Simba. Unajua kwanini? Kwasababu Omog ni kocha na anafanya kazi kwa kutumia weledi na akili lakini watu wa Simba wanatumia moyo katika kufikiri. Omog anafanya kazi, watu wa Simba wanataka ushindi tu, hawaelewi kingine.

Mwisho wa yote ukifanya tathmini ya kazi ya Omog, utagundua kuwa Simba inacheza pata potea dhidi ya kocha wa viwango vya juu. Achana na rekodi yake ya kushinda taji la kombe la Shirikisho Afrika, ndani ya Simba tu kocha huyo amefanya kazi kubwa.