Okwi aliamsha dude VPL

Straika wa Simba, Emmanuel Okwi

ETI upande wa pili wanadai straika wa Simba, Emmanuel Okwi ni muhenga? Mnakosea sana kwani, jamaa ni hatari sana anaposogelea goli la wapinzani. Okwi, ambaye kwa sasa amebeba matumaini ya Simba, anaziburuza klabu tano za Ligi Kuu Bara kwa idadi ya mabao.

Staa huyo wa kimataifa wa Uganda, amepachika mabao 16 mpaka sasa ambayo ni mengi kuliko klabu za Mtibwa Sugar yenye mabao 15, Ndanda (15), Kagera Sugar (13), Stand United (12) na Njombe yenye mabao 12.

Lakini, Lipuli ya Iringa na Majimaji ya Songea zimelingana kwa mabao na staa huyo. Makocha wa klabu hizo zinazoburuzwa na Okwi, wamefunguka kuwa kitendo cha kuzidiwa idadi ya mabao na mchezaji mmoja tu, ni somo jipya kwao.

Kocha msaidizi wa Njombe Mji, Mrage Kabange ambayo ina mabao 12 ikizidiwa manne na Okwi, amesema ndani ya kikosi hicho hakuna mchezaji anayefikia uwezo wa straika huyo. “Mchezaji mzoefu ndani ya kikosi chetu ni Ditram Nchimbi, lakini wengi ni wageni wa ligi, hivyo huwezi kufananisha na Okwi aliyecheza ndani na nje ya nchi,” alisema.

Kocha wa Lipuli, Amri Said alikiri kwamba ni aibu kubwa kushindwa kuwa na mabao ya kutosha kiasi cha kushindwa na mchezaji mmoja tu.

“Tunachukua rekodi hizo, tunawaonyesha wachezaji ili wapate uchungu wa kuona mtu mmoja anawaburuza safu nzima.

Alisema.Okwi anajituma kutokana na thamani yake kuanzia usajili hadi mshahara. Naye Athuman Bilali ‘Bilo’ wa Stand, alisema mafanikio ya Okwi yanatokana na ubora wa kikosi chake.