NINAVYOJUA: Nafurahi hii kasumba ya Usimba na Uyanga haipo

Joseph Kanakamfumu

KUMEKUWAPO na maneno mengi kwenye mitandao ya kijamii yanayozungumzia uteuzi wa wachezaji walioitwa kuitumikia timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, katika mechi mbili za kirafiki dhidi ya Algeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Michezo hii inaonekana kuwa mikubwa na mizuri kuwapima wachezaji wetu kuelekea michezo mingine ya kusaka tiketi ya Fainali za Afrika (Afcon) za mwakani, ambapo Stars ina kibarua cha kuvaana na Uganda na Cape Verde.

Kwa mtazamo huo, Kocha wa Taifa Stars ameona ni vema awaite wachezaji anaoamini wanafaa kujitayarisha kwa ajili ya michezo hiyo miwili ya Afcon.

Si rahisi kufanya uteuzi wa kikosi cha Stars kama utakuwa unayasikiliza maneno ya watu mbalimbali.

Kweli wapo wenye maono mazuri juu ya Stars yetu, lakini pia wapo wanaoingiza ushabiki zaidi kwenye uteuzi wa Stars.

Sawa, wakati mwingine pia ni vizuri kupitia mawazo yao mapema.

Ukiingia kwenye mitandao hiyo, utayaona mawazo kadhaa.

Wengi huyaangalia majina yaliyoteuliwa na kisha huanza kuwalinganisha wale wasiochaguliwa, lakini wanaonekana kuwa wazuri, pengine wanaoaminika kufanya vizuri kuliko hata wale waliochaguliwa.

Kwanza kuna mtazamo uliojengeka kwa Watanzania wengi kuwa wachezaji wengi wanaochaguliwa ni wale wanaozichezea Simba, Yanga na sasa Azam.

Mara nyingi wamekuwa wakienda mbali zaidi na kusema kuwa ukitaka kuichezea Stars, basi kwanza tafuta usajili kwa timu hizo mbili za Dar es Salaam.

Huko nyuma, nimewahi kukubaliana na uteuzi wa aina hiyo. Nilisema ni kutokana na Simba, Yanga na Azam kuwa na nguvu kubwa kiuchumi, hivyo ndio zinazosajili wachezaji wazuri katika soko la Kitanzania.

Nilisema siku zote Simba, Yanga tangu zamani na sasa Azam, ndizo huwa zinasajili wachezaji bora kutoka timu mbalimbali za nchini.

Timu kama Mtibwa na hata zamani Tukuyu Stars, Pamba, Coastal Union, zimekuwa zikiondokewa na mastaa wao wanaoishia Simba, Yanga na siku hizi Azam.

Ndio maana timu hizo zina mkusanyiko wa wachezaji bora wanaopata michezo mingi ya kimataifa na kuwafanya kuwa bora zaidi.

Kwa namna hiyo, ni rahisi kocha wa Stars kushawishika kuwateua kuingia katika timu yake na kuishia kuchomoa mmoja au wawili kutoka timu nyingine.

Hili si jambo la ajabu. Hata Ulaya mambo haya hutokea.

Ilishatokea hivyo kwa Waingereza wakati wa kizazi cha akina Philip Neville, Manchester United ilikuwa na karibu wachezaji saba kikosi cha kwanza cha England.

Kule Hispania mwaka 2010, walichukua Kombe la Dunia wakati timu ikitawaliwa na wachezaji wa Barcelona na Real Madrid.

Hata hivyo, angalau sasa kuna mambo yanaonekana kuwa si lazima mchezaji wa Simba, Yanga au Azam aitwe Taifa Stars.

Hii inaanza kuondoa dhana kuwa lazima mchezaji anapofanya vizuri tu ndani ya msimu wa kwanza au wa pili aitwe Stars, hapana.

Akina Pius Buswita, Yusuf Mlipili, Salmin Hoza na Idd Kipangwile, ni wachezaji wapya waliosajiliwa ndani ya Yanga, Simba na Azam na kwa yale mazoea yetu bila shaka tulitamani waitwe Stars, lakini hawakuitwa.

Kuna msururu wa wachezaji wengi nje ya Stars wanapigiwa chapuo waitwe.

Kwa mfano, kuna wachezaji wanaokipiga Ulaya, Wachezaji hawa ni Watanzania hasa na leo kesho wanataka kuja kuitumikia timu hii. Kuna wachezaji ambao ni damu changa wako Ukraine, Ujerumani, Uswisi, Sweden na kwingineko ambao wana uwezo wa kuitumikia timu hiyo.

Pia kuna akina Eliud Ambokile (Mbeya City), Jaffar Mohamed na Marcelo Kahenza (Majimaji), Mohamed Rashid (Prisons), Habibu Kyombo (Mbao) na wengine wengi tu ambao msimu huu ndio kwanza wameonekana na kufanya vizuri.

Wengi wao hawakuwahi kupitia hata timu za taifa za vijana, hawajacheza mchezo wowote ule wa kimataifa. Kwa ujumla hawana uzoefu huo, lakini watu wanataka waitwe kwenye Stars.

Wengi wa wachezaji wetu huwa hawana mwendelezo wa viwango bora kwa zaidi ya misimu miwili tu. Vijana wa kizazi hiki hawadumu kwenye ubora.

Ni wachezaji wanaofanya vizuri msimu mmoja kisha wa pili huwaoni.

Mfano ni Mfungaji Bora wa msimu uliopita, Abdulrahaman Mussa. Alikuwa moto msimu huo.

Kuna Mohamed Ibrahim na Mohamed Hussein wa Simba, yupo wapi Christopher Edward aliyecheza vizuri msimu uliopita?

Atupele Green, yule wa Ndanda aliyefunga magoli mengi tu na wengine wengi.

Kwa maana hiyo, wachezaji wengi wanaochipukia kwenye Ligi Kuu Bara na kuonekana kufanya vizuri msimu wao wa kwanza na hata wa pili, wanatakiwa kupewa muda zaidi ili wajijenge kwa faida ya nchi kabla ya kuanza kudhani wanafaa kuitwa Taifa Stars.