Miaka 10 ya Simba Day, rekodi za kibabe

LEO Jumatano Simba itashuka uwanjani kuvaana na Asante Kotoko ya Ghana katika mechi ya kuhitimisha Tamasha la Simba Day lililoasisiwa mwaka 2009.

Hii ni mechi ya 10 kwa Mabingwa hao wa soka wa Tanzania na mashabiki wanataka kuona mziki wa kikosi chao kilichoshuka nchini juzi Jumatatu kikitokea Uturuki kilipoweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya wa 2018-2019.

Mwanaspoti linakuletea orodha na matokeo ya mechi zote tisa za nyuma ambazo Simba imecheza tangu tamasha hilo lilipoasisiwa rasmi chini ya uongozi wa Mzee Hassan Dalali na Mwina Kaduguda. Rekodi zinaonyesha katika miaka 9 ya awali ya tamasha hilo, Simba imeshinda mara tano, ikipoteza mara tatu huku ikipata sare moja.

2009- Simba 1-0 SC Villa

Hili ndilo lililokuwa pambano la kwanza la ‘Simba Day’ na klabu hiyo ilivaana na SC Villa ya Uganda iliyoalikwa kulizindua tamasha hilo.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Uhuru (enzi ukiitwa Uwanja wa Taifa) na Simba kupata ushindi wa bao 1-0.

Bao hilo lilifungwa dakika ya 8 tu ya mchezo na kiungo Mkenya, Hilary Echessa, akiwa ndiyo kwanza amesajiliwa kutoka SC Villa. Kipindi hicho, Simba ilikuwa chini ya Kocha Mzambia Patrick Phiri. Na ndiyo msimu ambao Simba ilitwaa ubingwa bila kufungwa, huku nyota wa Uganda, Emmanuel Okwi na Joseph Owino walikuwa wamesajiliwa kwa mara ya kwanza.

2010- Simba 0-0 Express

Hii ndio mechi pekee ya Simba iliyoshindwa kutoa mshindi, kwani Simba ikiadhimisha mwaka wa pili wa tamasha hilo ililazimishwa suluhu na vijana hao wa Uganda na mechi ilipigwa Uwanja wa Uhuru, pia enzi ukiitwa Uwanja wa Taifa.

Kama ilivyokuwa kwenye msimu wa kwanza, safari hii pia Simba ilikuwa chini ya Phiri na iliundwa na nyota kama Ally Mustafa ‘Bathez’, Owino, Mohamed Banka, Rashid Gumbo, Okwi, Patrick Ochan, Shija Mkina, Amri Kiemba na Mussa Hassan Mgosi na Jerry Santo ambao hata hivyo, walishindwa kuwazidi ujanja Waganda.

2011- Simba 0-1 Victors

Kama ilivyokuwa kwa misimu miwili ya Simba Day, Wekundu hao wa Msimbazi waliialika pia timu ya Uganda, safari hii ilikuwa Victors na mechi ilipigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Kwa mara ya kwanza Simba ilipoteza mchezo mbele ya wageni wao hao kwa kulala bao 1-0. Bao hilo liliwekwa kimiani dakika ya 70 kwa mkwaju wa penalti na Patrick Sembuya, enzi hizo Kocha Mkuu wa Simba ni Mserbia Milovan Cirkovic.

2012- Simba 1-3 Nairobi City Stars

Wekundu wa Msimbazi chini ya Cirkovic iliendelea kuteseka kwenye tamasha lao kwa kulala mabao 3-1 kutoka kwa vijana wa Nairobi City Stars kutoka Kenya.

Pambano hilo la msimu wa nne lilipigwa kwenye uwanja wa sasa wa Taifa na mabao ya washindi yakiwekwa kimiani na Duncan Owiti dakika ya 57, Bruno Okullu dakika ya 69 na Boniphace Onyango aliyehitimisha dakika ya 79, huku bao la kufutia machozi la Simba likiwekwa kimiani na Mzambia, Felix Sunzu likiwa la kuongoza katika dakika ya 15.

2013- Simba 4-1 SC Villa

Kipigo cha Wakenya ni kama kiliwaamsha Simba na katika tamasha la mwaka huo, iliwaalika tena SC Villa na kuwashindilia mabao 4-1.

Pambano lilipigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa chini Kocha Abdallah Kibadeni aliyechukua nafasi ya Cirkovic na chipukizi wa kipindi hicho Jonas Mkude alifungua pazia kwa bao la dakika ya 43 kabla ya William Lucian ‘Gallas’ naye kuongeza la pili dakika ya 53. Mkongwe Betram Mombeki aliyefunga mabao mawili katika dakika ya 70 na 72.

2014- Simba 0-3 Zesco

‘TANESCO’ ya Zambia, Zesco FC ilifanya kufuru kwa kuitibulia Simba sherehe kwenye tamasha hilo la sita kwa kuinyoosha kwa mabao 3-0, enzi hizo timu ikiwa chini ya Kocha Mcroatia Zdravko Logarusic.

Wazambia hao walipata mabao yao kupitia kwa Jackson Mwanza dakika ya 14, Cletus Chama dakika ya 64 kwa penalti na Mayban Mwamba dakika ya 90. Chama ndiye kiungo mpya wa Msimbazi anayetarajiwa kutambulishwa jioni ya leo pale Taifa.

2015- Simba 1- 0 SC Villa

Tamasha la saba ya Simba Day liliishuhudia SC Villa ikirudi tena nchini kwa mara ya tatu kuvaana na Simba na kama kawaida iliendelea kuwa mdebwebo kwa kufungwa bao 1-0. Bao pekee la Simba liliwekwa kimiani na kiungo Awadh Juma katika dakika ya 89 wakati mashabiki wa Msimbazi wakiwa wameshaanza kutoka Uwanja wa Taifa kwa kuamini mechi imeisha kwa suluhu.

2016- Simba 4-0 AFC Leopards

Katika mchezo huu uliokuwa wa nane kwa Simba kuadhimisha siku yao, walipata ushindi wa kishindo kwa kuigagadua, AFC Leopards ya Kenya kwa mabao 4-0.

Ibrahim Ajibu ndiye aliyekuwa shujaa wa mchezo huo kwa kufunga mabao mawili katika mechi hiyo ya Tamasha la Nane, huku straika Mrundi aliyekuwa amejiunga na timu hiyo akitokea Vital’O, Laudit Mavugo naye alitupia moja kambani.

Bao jingine liliwekwa na winga, Shiza Kichuya aliyekuwa akiicheza Simba kwa mara ya kwanza akitokea Mtibwa Sugar na kuhitimisha ushindi mnono.

2017- Simba 1-0 Rayon Sports-2017

Mechi hii iliyopigwa mwaka mmoja uliopita ilishuhudia Simba ikitakata kwa kuifumua Rayon Sports ya Rwanda bao 1-0.

Kiungo Mohammed Ibrahim ndiye aliyewazima Wanyarwanda kwa kufunga bao pekee la mchezo huo katika dakika ya 15 baada ya kupokea pasi nzuri ya Emmanuel Okwi aliyeingia kwa kasi katika eneo la hatari.

2018- Simba v Asante Kotoko?

PAMBANO hili linalochezwa jioni ya leo linasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa Simba kwa sababu ni mara yao ya kwanza kuishuhudia timu yao ikiialika klabu kubwa kutoka Afrika Magharibi kuja kunogesha tamasha hilo.

Hii inakuwa timu ya pili kutoka nje ya Afrika Mashariki kuja kunogesha Simba Day baada ya Zesco ya Zambia, timu nyingine zimekuwa zikitoka Afrika Mashariki katika nchi za Kenya, Uganda na Rwanda.