Mbeya City kwani vipi wana?

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, alisema kuwa wameamua kufanya hivyo baada ya kufanya tathimini ya kina ya kipato kwa kutazama kile wanachoingiza na wanachotumia na kugundua kuwa wanajiingiza kwenye jukumu kubwa ambalo linakuwa mzigo kwa klabu.

VIGOGO wa soka wa Nyanda za Juu Kusini, Mbeya City nao wameingia kwenye mfumo wa kupunguza gharama za uendeshaji wa klabu hiyo ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mbeya City nao wameamua kufanya hivyo baada ya kupungua kwa vyanzo vya mapato ambavyo walikuwa wakivitegemea, ambapo sasa usajili wao utakuwa ni bure ama wa gharama nafuu.

Imebainika kwamba mchezaji atakayehitaji kusajiliwa na timu hiyo inabidi akubaliane na hali halisi ya kupewa pesa kidogo ya usajili pamoja na mshahara wa kawaida, jambo ambalo baadhi ya mastaa wao kama Ditram Nchimbi wameligomea na kuondoka.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, alisema kuwa wameamua kufanya hivyo baada ya kufanya tathimini ya kina ya kipato kwa kutazama kile wanachoingiza na wanachotumia na kugundua kuwa wanajiingiza kwenye jukumu kubwa ambalo linakuwa mzigo kwa klabu.

Kimbe alisema kwa sasa wanatazamia kuwa na hali ngumu lakini wanaamini hapo baadaye wakikamilisha mchakato wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kwenda kwenye mfumo wa hisa, wataanza kupata pesa itakayokidhi mahitaji yao.

“Tulikuwa tunatumia gharama kubwa sana kuliko kile kinachoingia na hii imefanyika kwa kipindi kirefu, sasa hivi mambo yamebadilika ndiyo maana tumepunguza gharama za uendeshaji, kila sehemu tumepunguza matumizi,” alisema.