Mayay, Mogella: Kagere hawezi kuvunja ufalme wa Okwi

Muktasari:

  • Kagere tangu ametua Simba msimu huu tayari amefunga mabao matatu katika michezo mwili wakati Okwi mfungaji bora wa msimu uliopita akiwa hajafunga.

Dar es Salaam. Kasi kubwa aliyoanza nayo mshambuliaji Meddie Kagere imeanza kutia shaka uenda akaupoteza ufalme wa Emmanuel Okwi iwapo atafunga bao katika mechi ya watani jadi Simba na Yanga hapo Septemba 29.

Kagere tangu ametua Simba msimu huu tayari amefunga mabao matatu katika michezo mwili wakati Okwi mfungaji bora wa msimu uliopita akiwa hajafunga.

Akizungumzia suala hilo nyota wa zamani wa Yanga na timu ya taifa 'Taifa Stars' Ally Mayay amesema Kagere hawezi kuvunja ufalme wa Okwi aliojitengenezea katika klabu hiyo.

Mayay alisema Okwi tayari ameshajitengenezea ufalme katika kikosi hicho kwa kukutana na changamoto nyingi na kufanikiwa kuzifanyia kazi na kuweka wazi kuwa hilo kwa Kagere bado halijafanyika pamoja na kuisaidia timu yake kupata ushindi katika michezo miwili ya ligi.

"Kagere ni mzuri sana kufumania nyavu hilo halina ubishi, lakini bado hana nafasi ya kuchukua ufalme wa Okwi ni kutokana na mashabiki wa timu hiyo kushindwa kukosa uvumilivu kwani kwa sasa anafanya vizuri anaonekana kupewa sifa, lakini akikosea mara moja tu ndio atakapojua ugumu wa timu hiyo kutokana na kutolewa maeno makali na mashabiki wake wanaompa sifa sasa," alisema.

"Okwi changamoto hiyo tayari ameshaipitia na sasa amekuwa mchezaji hata akikosea anaambiwa ni bahati mbaya kwa sababu tayari wameshajua ni mchezaji ambaye hawezi kufanya kosa makusudi kutokana na mapenzi yake kwa timu hiyo," alisema Mayay.

Naye mshambuliaji wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alisema kila mchezaji anauchezaji wa tofauti na kila mmoja anakubalika kwa mashabiki kutokana na uchezaji wake.

"Okwi bado ajapata nafasi ya kucheza katika ligi Kagere kashacheza na kujitengenezea nafasi ya kufunga mabao katika michezo yote aliyocheza kuna baadhi wanaompenda Okwi wanasema kafunga kwa sababu hayupo hivyo tumpe nafasi mwalimu kama ataweza kuwatumia wote wawili tutajua nani ni bora zaidi ya mwingine," alisema Mogella.

Mogella alisema anaamini wachezaji wote ni bora na wanaweza wakuisaidia Simba kwa nyakati tofauti na kuweka wazi kuwa ataendelea kuamini uwezo wa kila mmoja pale anapoisaidia timu iweze kufikia mafanikio.