Mavugo akitoka tu, jamaa anatua Simba

Muktasari:

>> Habari za ndani kutoka Simba ni kwamba kumekuwa na mvutano baina ya vigogo wa Simba kuhusu kumruhusu Mavugo aondoke

SIKU nne kabla ya dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu Bara halijafungwa, straika Mrundi, Laudit Mavugo,  ameiweka Simba njia panda juu ya hatma ya kumsainisha straika mkongwe kutoka Zambia, Jonas Sekuhawa.

Mzambia huyo mwenye umri wa miaka 34 aliyewahi kuzichezea klabu za TP Mazembe na Zesco United, Ijumaa iliyopita alifanya yake baada ya kuifungia Simba bao moja walipoichapa KMC mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki.

Sakuhawa kwa sasa anamsubiri tu Kocha Mkuu, Joseph Omog atue kutoka Cameroon ili ajue hatma yake ambapo kama Mrundi Laudit Mavugo ataruhusiwa kutimka Msimbazi, basi Mzambia huyo kiulaini atapewa mkataba wa kuichezea Simba hata kwa nusu msimu, kwani ameonekana ni mmoja ya wachezaji wazoefu na mwenye uwezo, japo kikwazo kinaweza kuwa umri alionayo.

Habari ambazo hazina shaka ni kuwa Sakuhawa amemkuna Kocha Msaidizi, Masudi Djuma na wanasubiri maamuzi ya bosi wake Omog, lakini kubwa likiwa ni kujua namna mabosi wa Simba watakavyomalizana na Mavugo.

Mabosi wa Simba wapo katika tafakari ya kumuacha Mavugo anayetakiwa na Gor Mahia, huku pia wakipiga hesabu za kumkata beki nahodha wao, Method Mwanjali lakini wanapata wasiwasi kuwa huenda beki yao ikapwaya wakati wa mashindano ya kimataifa mwakani.

MVUTANO

Habari za ndani kutoka Simba ni kwamba kumekuwa na mvutano baina ya vigogo wa Simba kuhusu kumruhusu Mavugo aondoke, kwani hawataki kukipangua kikosi hata kama wanavutiwa na uwezo wa Sakuhawa.

“Mavugo ndiye aliyeshikilia hatma ya Mzambia, kama Omog ataridhia asajiliwe maana yake Mavugo ataondoka, ikishindikana Sekuhawa na Mavugo wataungana pamoja na Mwanjali ataachwa,” chanzo ndani ya Simba kililidokeza Mwanaspoti.

BENCHI LANENA

Kocha Msaidizi, Djuma alisema amemuona Sakuhawa ni mchezaji mzuri ambaye ana utulivu katika eneo la kufunga, mzoefu anayeweza kuwabeba kimataifa, ila wanaendelea kumuangalia kabla ya kumsainisha mara Omog atakapokuja.

“Naendelea kumuangalia kwani kwa wiki moja amenionyesha ana kitu na anaweza kutusaidia,” alisema Djuma.

Naye Meneja wa Simba, Richard Robert alielezea kuridhishwa na Sakuhawa.

“Makocha ndio wenye maamuzi ya mwisho, ndio wanaoona zaidi mambo ya msingi kutokana na aina ya mchezaji wanayemhitaji,” alisema Robert.