Mastaa wapya ambao bado hawajacheza hata dakika England

Muktasari:

Hata hivyo, kuna baadhi ya wachezaji waliowanunua mpaka leo hawajagusa uwanjani katika mechi za Ligi Kuu ya England.

DIRISHA la uhamisho wa mastaa lilipowadia baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, makocha na mabosi wa timu mbalimbali waliingia sokoni kuimarisha vikosi vyao.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wachezaji waliowanunua mpaka leo hawajagusa uwanjani katika mechi za Ligi Kuu ya England.

Bernd Leno (kipa, Arsenal)

Alinunuliwa kwa dau la Pauni 19.2 milioni kutoka Bayer Leverkusen na alitazamiwa moja kwa moja kuwa kipa namba moja wa Arsenal baada ya Petr Cech kuonekana kubabaisha msimu uliopita. Hata hivyo, Kocha mpya wa Arsenal, Unai Emery ameamua kuendelea kumwamini Cech na kumpiga benchi Leno mwenye umri wa miaka 26. Awali Leo alikuwa kipa wa kudumu Leverkusen kwa misimu saba huku akicheza mechi zaidi ya mechi 300 katika klabu hiyo ya Ujerumani. Kitu kibaya zaidi kwa Leno, anaonekana kuwa fiti lakini Emery ameamua tu kumsugulisha. Inaonekana kwa sasa atalazimika kusubiri mpaka Cech afanye makosa ya wazi ndipo apate nafasi yake.

Ben Gibson

(beki, Burnley)

Mlinzi wa shoka ambaye alinunuliwa kwa Pauni 15 milioni kutoka Middlesbrough ambako alikuwa nahodha. Alionekana kama angeingia moja kwa moja katika mipango ya Kocha Sean Dyche baada ya kuvunja rekodi yao ya uhamisho lakini inaonekana ameshindwa kuing’oa kombinesheni ya walinzi James Tarkowski na Ben Mee mpaka sasa. Walinzi hao kwa kiasi kikubwa walipongezwa kwa mafanikio ya Burnley msimu uliopita. Pamoja na kutocheza mpaka sasa, kikosi cha Burnley kinaonekana kidogo na kuna uwezekano mkubwa akaonekana uwanjani muda mfupi ujao.

Andre Gomes

(kiungo, Everton)

Everton wametoa Pauni 2 milioni kwa ajili ya kupata huduma za Gomes kwa mkopo. Ni mmoja kati ya wachezaji wenye vipaji lakini amekuwa na tatizo la kukosa nafasi katika klabu kubwa kama vile Barcelona alikotoka.

Hakuwepo katika kikosi cha Ureno kilichoshiriki michuano ya kombe la dunia nchini Russia mapema mwaka huu na inawezekana idadi ya mechi chache alizochezea Barcelona msimu uliopita ilichangia. Alicheza mechi 16 tu za La Liga. Amejiunga na Everton kwa ajili ya kujaribu kuwa fiti tena lakini majeraha ya misuli yamemweka nje na tunaweza kumwona akiichezea Everton wiki chache zijazo. Mpaka sasa hajagusa uwanjani.

Yerry Mina (Beki, Everton)

Alinunuliwa kwa dau la Pauni 26.8 milioni akitokea Barcelona baada ya kutamba katika michuano ya Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Colombia ambacho alikifungia mabao matatu. Mina anaungana na Gomes kusugua benchi Everton wakitokea Barcelona. Pamoja na maumivu ya mguu kumfanya asicheze mechi yoyote mpaka sasa lakini inadaiwa anaweza kucheza mechi ya wikiendi hii dhidi ya West Ham pale Goodison Park.

Sergio Rico (Kipa, Fulham)

Mmoja kati ya makipa maarufu katika soka ya Hispania ambaye ametua England kwa mkopo akikipiga katika klabu ya Fulham ya London.

Alitwaa mara mbili michuano ya Europa na Sevilla lakini msimu uliopita kipa huyu wa timu ya taifa ya Hispania alianza kuwekwa benchi na kipa wa vijana, David Soria baada ya timu hiyo kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Rico pia alikorofishana na kocha wake, Vincenzo Montella na hivyo kuzuka kwa uvumi angeondoka klabuni hapo.

Hata hivyo amekwenda Fulham ambako upinzani katika nafasi yake ni mkubwa akikutana na kipa, Marcus Bettinelli pamoja na kipa wa zamani wa Besiktas, Fabri. Kama Bettinelli ambaye ndiye anacheza ataendeleza fomu yake basi huenda kipindi cha mkopo cha Rico kikawa kibaya London.

Fabinho (Liverpool)

Mashabiki wa Liverpool bado wana hamu ya kumwona staa huyu wa kimataifa wa Brazil ambaye klabu yao ililipa Pauni 30 milioni kwenda Monaco kwa ajili ya kupata huduma zake. Liverpool walihitaji mchezaji wa kuulinda ukuta wao na Fabinho alikuwa mchezaji wa kwanza kununuliwa. Sio tu kwamba ni mlindaji wa ukuta lakini ana uwezo mkubwa wa kufunga na alifunga mabao 20 katika misimu yake miwili iliopita akiwa na Monaco kiasi cha kuzilazimisha timu kubwa kumwania. Haijulikani kwa nini bado hachezeshwi lakini kitendo chake cha kukaa benchi Anfield kimeanza kuathiri nafasi yake katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil. katika pambano la kirafiki dhidi ya Marekani, Fabinho alichezeshwa kama mlinzi wa kulia wakati kiungo mpya wa Manchester United, Fred alichezeshwa kama kiungo wa kati.

Diogo Dalot

(Beki, Man United)

Anaonekana kama mchezaji ambaye anaandaliwa kuwa staa au mchezaji muhimu katika misimu inayokuja lakini watu wengi waliamini kinda huyu angeweza kuwa mchezaji muhimu hata msimu huu.

Alinunuliwa kwa Pauni 19 milioni kutoka Porto na Kocha Jose Mourinho alimwagia sifa lukuki mara baada ya kukamilika kwa uhamisho huo. Mlinzi wa kulia, Antonio Valencia ana umri wa miaka 33 na umri wake haurudi nyuma tena.Hapo ndipo Diogo (19) anaweza kuwa muhimu.

Hata hivyo, kwa kipindi kirefu Diogo alikuwa ameumia. Alirudi katika mechi ya wachezaji wa akiba wikiendi iliyopita na kuonyesha kiwango bora.

Inaonekana muda si mrefu anaweza kupambana na nahodha wake Old Trafford ingawa mpaka sasa hajagusa mechi yoyote ya Ligi Kuu. Tatizo kubwa ni rekodi ya Mourinho katika kuwaamini wachezaji chipukizi. Inatia shaka.

Leander Dendoncker (Beki, Wolves)

Moja kati ya usajili ambao uliwafurahisha mashabiki wengi wa Wolves. Dendoncker alitua klabuni hapo katika dirisha kubwa la majira ya joto akitokea klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji kwa mkopo. Hii ilikuja baada ya mlinzi huyo wa kulia kung’ara katika michuano ya Kombe la Dunia, Russia akiwa na kikosi cha Ubelgiji. Akiwa na umri wa miaka 23 aliichezea Anderlecht mechi 171 huku mechi zake sita kwa timu ya taifa ya Ubelgiji zikija wakati wa michuano ya kombe la dunia.

Dendoncker, ambaye pia anaweza kucheza kiungo mkabaji ameichezea Wolves mechi moja tu ya kombe la Ligi huku kikosi chao kikionekana kuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu na wengine vijana wenye vipaji.

Anahitaji kufanya kazi kubwa kutamba Ligi Kuu ya England kama ambavyo wachezaji wengi wa kikosi chao cha Ubelgiji wanavyotamba. Kama amechukuliwa kwa ajili ya kutumika kama mchezaji wa kiungo basi atapata wakati mgumu kutoka kwa mkongwe wa Ureno, Joao Moutinho pamoja na kipaji kingine cha Kireno kinachokuja kwa kasi, Ruben Neves.