Masau Bwire avuna umaarufu vijijini Mtwara

 KUANZIA halmashauri ya Newala mjini yenye kata  16 hadi vijijini katika tarafa za Mchemo, Mkwedu, Chilangala, Kitangali mkoani Mtwara jina la msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire limetawala midomoni mwa watu.

Yule ndiyo mzee wa kupapasa Masau ambaye amewafanya wapenzi  hao wa soka kuwa wanachama wapya wa Ruvu Shooting ambao  walikuwa wakimiminika  kila msafara huo ulipokuwa ukikatisha.

Masau  'mzee wa kupapasa' ndiye aliyeongoza uzinduzi wa tawi lao jipya  la  Makonga chini ya Mwenyekiti, Hamisi Mmalunda na makamu wake, Hamisi Laini huku kukiwa na mamia ya wachama wapya.

Msemaji huyo, alitumia nafasi hiyo kuongea na wanachama hao kwa kusema msimu huu wa Ligi Kuu Bara wamekuja na mfumo mpya wa kupapasa kwa kila hali na kila eneo 'papasa square'.

"Maamuzi yenu ya kuachana na hizo timu nyingine yametugusa na kuamua kuja kuweka historia hapa, tunawashukuru sana kwa kuwa sehemu ya familia ya Ruvu Shooting kwa kila namna tutawapapasa," alisema Masau.

Mapokezi ya Ruvu Shooting ambao wataanza safari leo ya kurejea Pwani yalikuwa makubwa yakiongozwa na  Mkuu wa Wilaya ya Newala, Bi Aziza Mangosongo.

 

Mkuu huyo wa Wilaya alimpa heshima ya aina yake Masau kwa  kumgharamikia  malazi katika hotel kubwa ya Kitalii nje kidogo ya mji wa Newala.