Mambo yaiva wanariadha wa kusaka medali Madola

Muktasari:

Barie alisema baada ya kukabidhiwa bendera watajumuika na wenzao kwa ajili ya safari kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wiki ijayo.

TIMU ya riadha inayokwenda kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola inatarajia kuondoka mkoani hapa Keshokutwa Jumapili kwenda Dar es Salaam kuungana na timu za michezo mingine lakini kocha wa timu hiyo, Zakaria Barie ametoa neno la mwisho kabla ya kupaa.

Barie alisema baada ya kukabidhiwa bendera watajumuika na wenzao kwa ajili ya safari kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wiki ijayo.

“Tumepata kila kitu kwa muda tuliokuwa kambini tangu Februari 8 wakati kambi ikiwa na wanariadha 15 na baadaye tukabaki tisa baada ya wengine kuondoka, kila kitu kimeenda vizuri na matumaini ya kufanya vizuri yapo,” alisema Barie.

Kocha huyo aliongeza hadi sasa hakuna mwanariadha mwenye matatizo ya kiafya na wote wapo tayari kushindana kwenye mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Aprili 4.

Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo, Said Makula aliwaondoa wasiwasi Watanzania kwa kueleza kuwa watakwenda kufanya vizuri kwenye mashindano hayo licha ya changamoto zilizojitokeza hapo nyuma.

“Kila mtu anawaza lake kuhusu mashindano haya lakini siri kubwa ya mwanariadha ni kujiaandaa kwa asilimia 75 huku zilizobaki ndizo zinakuwa za kocha,” alisema Makula.

Wanariadha wanaotarajiwa kwenda kupeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano hayo ni Stephano Huche, Said Makula na Sara Ramadhan kwa upande wa mbio ndefu, wengine ni Failuna Abdi (mita 10,000), Ally Gulam wa (mita 100) na 200 na Anthony Mwanga wa mbio za miruko.