Liverpool ya Fekir nakwambia wapinzani watakohoa damu

DILI la Nabil Fekir kwenda Liverpool linakaribia kukamilika na taarifa za kutoka Ufaransa zimedai kwa asilimia 99 kila kitu tayari, kimekamilika.

Kwa hali ya mambo ilivyo ni wazi kabisa, staa huyo wa Ufaransa atakuwa amecheza mechi yake ya mwisho huko Lyon na msimu ujao atakuwa kwenye kikosi cha wababe wa Anfield. Kwenye mikimikimiki ya msimu huu ikiwamo Ligue 1, Fekir alifunga mabao 23 katika mechi 40 na hakika kiwango chake bora cha ndani ya uwanja kimemfanya kuwa tishio kwelikweli kwa mabeki wa upinzani hivyo, Kocha Jurgen Klopp atawafanya kitu mbaya wapinzani wake kwa msimu ujao.

Kwa fowadi yake ya sasa tu yenye mastaa Sadio Mane, Roberto Firmino na Mohamed Salah imekuwa matata na moto wa kuotea mbali, je, akija Fekir, si wapinzani watakohoa damu uwanjani, maana itakuwa kukimbizwa mwanzo mwisho.

Lakini, swali la kujiuliza na ambalo linasumbua vichwa vya waliowengi, kwa kikosi cha Liverpool kuanzia kwenye kiungo kwenda mbele pamoja na usajili mwingine itakaofanya kwa sababu Naby Keita, naye atatua kwenye kikosi hicho, je, Fekir atafiti wapi?

Cheki hapa mitindo mitano tofauti ya kiuchezaji ambayo Klopp atatumia msimu ujao baada ya ujio wa Fekir kwenye kikosi chake.

1. Kushambulia mwanzo mwisho

Unakumbuka ule msemo wa Nne Takatifu? Basi ndivyo itakavyokuwa msimu ujao. Kwa namna fulani msimu uliopita, Klopp alitumia fowadi ya wanne takatifu, alipowatumia Salah, Philippe Coutinho, Mane na Firmino kabla ya mmoja wao kuondoka na kubaki na fowadi watatu.

Lakini, kwa ujio wa Fekir, ile fowadi ya wakali wanne itarudi na hapo ndipo patakapokuwa patamu kwa sababu safari hii kwenye kiungo kutakuwa na mtu anayeitwa Naby Keita, ambaye ni moto kwa pasi za mwisho na wakati wote anakimbilia kwenye sehemu hatari za wapinzi. Hakuna namna, Klopp hapo atatumia fomesheni ya 4-3-3, ambapo kwenye wale viungo watatu wa kati, kutakuwa na Keita, Fekir na Jordan Henderson.

2.Kucheza kushoto zaidi

Kwenye mtindo huu, Klopp anaweza kuwa na staili ileile ya 4-3-3, lakini tofauti yake hapa ni kwamba Fekir atakuwa upande wa kushoto kwenye kushambulia zaidi, huku Sadio Mane nyuma yake kwa ndani kidogo, ambapo atakuwa na kazi ya kupokea mipira kutoka kwenye kiungo ya Keita na Henderson. Unaweza ukasema hilo litakuwapo, lakini kimsingi kwa msimu uliopita, mara kadhaa Mane alionekana akiondolewa kwenye ile fowadi ya wakali watatu, akishambulia kutoka kwenye kiungo, kumwaacha Giorginio Wijnaldum kushambulia akitokea pembeni, hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa Fekir.

3.Mechi za ugenini

Kocha Klopp wakati mwingine kwenye mechi zake za ugenini amekuwa akicheza fomesheni ya 4-2-2-2, kwa maana ya kuwa na viungo wanne katikati, ambao waliogawanyika wawili wawili, huku kule mbele kuwa na washambuliaji wawili.

Nyakati ambazo alitumia mfumo huo ugenini kwa Stoke City na West Ham United alishinda 3-0 na 4-1.

Kwa ujio wa Fekir, kama Klopp atataka kutumia mfumo huo, basi atamtumia Mfaransa huyo kwenye upande wa kushoto na Mane atakuwa upande wa kulia, huku Salah na Firmino watakuwa katikati kwenye kushambulia. Hapo kwenye ile safu ya kiungo, wakali watakaokuwa hapo ni viungo Wijnaldum na Keita na hapo Henderson itabidi asubiri tu kwenye benchi.

4.Nyuma ya Roberto Firmino

Kuna nyakati, Klopp amekuwa akichukua uamuzi wa kumtumia Dominic Solanke mbele ya ile safu yake ya washambuliaji watatu, yaani Mane, Firmino na Salah wanacheza nyuma ya straika huyo. Lakini, kwa ujio wa Fekir, hapo Solanke atapaswa kukaa benchi na Firmino atatangulizwa akicheza straika huku nyuma yake, Mane atakuwa kushoto, Salah kulia na Fekir atasimama katikati, nyuma ya mshambuliaji wa kati, ambaye ni Firmino. Kutokana na kuwa na kikosi kilichojaa wakali, ujio wa Keita utamfanya Klopp kuwa na kikosi chenye uimara katika kila idara.

Kwenye kiungo kutakuwa na Henderson na ama James Milner au Keita kuhakikisha mabeki wa kati wanakuwa salama.

5.Sadio Mane benchi

Pengine kuongezeka kwa Fekir kwenye kikosi hicho ni mpango wa Klopp wa kutaka kikosi chake kiwe na umiliki mkubwa zaidi wa mpira kuanzia mbele na kupunguza matumizi ya nguvu badala ya ufundi.

Kumtumia Fekir kwenye Namba 10, staili ya diamond, kutaifanya Liverpool kuwa na uhai mkubwa zaidi pengine kuliko hata inapocheza staili hiyo ikiwa na Mane uwanjani, hivyo hapo staa huyo wa Senegal itabidi aanzie kwenye benchi.

Kwenye mfumo huo, Klopp mchezaji mwingine ambaye anaweza kumwingiza kikosini basi anaweza kuwa Alex Oxlade-Chamberlain au Adam Lallana, ambao watacheza upande wa kulia. Kwenye kiungo kutakuwa na Keita na kule mbele Fekir atawasapoti Firmino na mkali Salah.