Kumekucha kwenye wavu Dar

Muktasari:

  • Hatua hiyo ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa mchezo huo ilianza rasmi Ijumaa iliyopita kwa michezo kadhaa kupigwa.

Dude limeamshwa kwenye michuano ya mpira wa Wavu Dar kwa IP Sports kutoa dozi mfululizo kwenye hatua ya mchujo (Play Off) ambayo inaendelea, DIT.

Hatua hiyo ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa mchezo huo ilianza rasmi Ijumaa iliyopita kwa michezo kadhaa kupigwa.

Muundo wa michuano hiyo upo kwenye hatua ya mwisho baada ya kuchezwa hatua ya kwanza na kupatikana timu nne bora kwa wanaume na wanawake ambazo zinachuana tena kupatikana bingwa kwa mfumo wa Ligi.

Kufuatia kupata kwao matokeo ya ushindi kwenye michezo 2 mfululizo na kuongoza kwa Pointi 6 kwa wanaume, nahodha wa IP Sports, Charles Okare alisema wamepania kutwaa ubingwa.

Mbali na IP Sports kuongoza kwa wanaume kwa utofauti wa seti za kushinda na kufungwa lakini pia Tanzania Prisons ya wanawake inaongoza upande wa pili kwa kuwa na Pointi 6.