Kocha Prisons anataka fowadi matata

KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Abdallah Mohamed, amesema licha ya mipango ya mabosi wake kutaka wasajili wachezaji zaidi ya watatu, yeye anaumiza kichwa kumpata mchezaji atakayeiwezesha timu kupata matokeo.

Akizungumza jana Jumatano mara baada ya kumalizika kwa mechi yao ya kirafiki dhidi ya Mbeya Kwanza iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2, Mohamed alisema benchi lake linapenda kusajili fowadi mmoja matata.

Alisema dhamira kubwa na macho yake anayaelekeza kumpata mchezaji huyo kutoka jijini Dar es Salaam, ingawa hakuwa tayari kutaja jina wala timu anayotoka mchezaji huyo.

“Umaliziaji kwa misimu miwili limekuwa  ni tatizo linalonisumbua na kuinyima timu matokeo mazuri, hivyo saa chache zilizobakia kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa nataka nilishughulikie hilo na kumalizana na straika huyo,” alisema.

Alisema akimpata fowadi huyo anaamini atasaidiana na waliopo na nafasi zilizosalia ataendelea kuwapa wachezaji wa kikosi cha vijana anaowaamini.

‘’Tunataka pia mchezaji wa kiungo na huyo tunaweza kumpata katika timu yetu ya vijana wa umri chini ya miaka 20 ili aweze kuungana na wachezaji wenzake katika kuisaidia timu hii kufanya vizuri katika Ligi Kuu msimu huu,” alisema.

Prisons ni ya sita katika msimamo ikiwa na alama 15 baada ya kucheza mechi 11.